……………………………………………………………………………………
Na.Richard Boniphance,Dodoma
BARAZA la Maaskofu kanisa la E.A.G.T Tanzania wamempongeza Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa uongozi imara wa serikali ya awamu ya tano.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Askofu Mkuu wa kanisa la E.A.G.T Dkt. Brown Mwakipesile,wakati wa mkutano mkuu wa baraza la maaskofu Nchi nzima,amesema kuwa kwa pamoja wamekutana katika mkutano huo muhimu kwa lengo la kujadili na kupongeza jitihada za serikali ya awamu ya tano kutokana na ujasiri na ushujaa ambao Rais Dkt. John Pombe ameudhihirishia ulimwengu katika kupambana na ugonjwa hatari wa COVID-19.
“Rais alikuwa mfariji mkuu wa taifa la Tanzania haswa kwa kumtanguliza mungu mbele kuliko kitu kingine katika kupambana na janga ambalo limeitetemesha dunia kwa kiasi kikubwa lakini kiongozi wetu alikuwa mstari wa mbele kuhimiza watu wasali na kuliombea taifa kwani mungu pekee ndiyo mwenye uwezo wa kutukinga na janga hili” amesema Mwakipesile
Awali akisoma taarifa, Askofu Mkuu wa Kanisa la E.A.G.T Tanzania Dkt. Brown Mwakipesile aliongeza kuwa amani iliyopo Nchini ni kubwa na ni kwa uweza wa mungu pekee hata wameweza kukutana na kufanya mkutano kama maaskofu Nchi nzima kutokana na ujasiri na ushujaa wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania katika kuhakikisa Nchi yetu inakuwa salama hata wakati wa kipindi hiki kigumu cha vita dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona.
Aidha, aliongeza kuwa maendeleo makubwa yamefanyika ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo ni pamoja na ujenzi wa Reli mpya ya kisasa (standard Gauge) miradi ya umeme, barabara, hospitali, shule, zahanati, madaraja nk.
Kwa upande wako, wawakilishi wa maaskofu kutoka majimbo mbalimbali akiwemo Askofu wa kanda ya nyanda za juu kusini mashariki, Askofu Cassian Kayombo na Askofu wa jimbo la Mbarali Elia Sembeye wamesema kuwa matarijio yao ni makubwa kwa siku za usoni kwani uongozi wa Rais Magufuli pamoja na timu yake yote ni thabiti na imara tangu hapo walipo kabidhiwa Nchi mpaka sasa wameonyesha mabadiliko makubwa sana katika ulimwengu wote.
Baraza hilo hukaa mara moja kwa mwaka, lengo ikiwa ni kujadili maendeleo licha ya kujitokeza kwa maradhi ya COVID 19 ugonjwa uliotishia kudorora kwa hali ya uchumi katika mataifa mbalimbali. Hata hivyo Tanzania imeendelea kusimama imara na kupiga hatua licha ya uwepo wa maradhi hayo Nchini.