Home Mchanganyiko Barabara za lami katika Mji wa Serikali kugharimu zaidi ya Bilioni 89

Barabara za lami katika Mji wa Serikali kugharimu zaidi ya Bilioni 89

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff kuhusu mradi wa ujenzi wa Barabara za lami zenye jumla ya km 51.2 katika mji wa Serikali (Mtumba) mkoani Dodoma leo tarehe 11 Juni 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo wakivuta utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la Msingi mradi wa ujenzi wa Barabara za lami zenye jumla ya km 51.2 katika mji wa Serikali (Mtumba) mkoani Dodoma leo tarehe 11 Juni 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi wakati Bendi ya JKT Makutopora ilipokuwa ikitumbuiza kabla ya kufungua jengo la Ofisi za Makao Makuu ya TARURA mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, Waziri wa Ardhi William Lukuvi katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Wizara wa Ardhi mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Barabara za lami zenye jumla ya km 51.2 katika mji wa Serikali (Mtumba) mkoani Dodoma leo tarehe 11 Juni 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi mara baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa Barabara za lami zenye jumla ya km 51.2 katika mji wa Serikali (Mtumba) mkoani Dodoma leo tarehe 11 Juni 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mitambo itakayotumika katika katika ujenzi wa Barabara za lami zenye jumla ya km 51.2 katika mji wa Serikali (Mtumba) mkoani Dodoma leo tarehe 11 Juni 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili katika viwanja vya Makao Makuu ya Ofisi za TARURA Mtumba mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama pamoja na viongozi wengine ili kumkumbuka Marehemu Pierre Nkururinza Rais wa zamani wa Burudi aliyefariki juzi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wafanyakazi mbalimbali wa Serikali kabla ya kufungua Jengo la Ofisi za Makao Makuu ya TARURA mjini Dodoma.

Baadhi ya Makatibu Wakuu wakiwa katika hafla fupi ya ufunguzi wa Jengo la Ofisi za Makao Makuu ya TARURA mjini Dodoma

Baadhi ya Wafanyakazi wa Serikali wakiwa katika viwanja vya Mtumba kwenye hafla ya ufunguzi wa Jengo la Ofisi za Makao Makuu ya TARURA mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiendesha moja ya pikipiki ambazo alizikabidhi kwa Maafisa Tarafa wa nchi nzima katika hafla ya ufunguzi wa Jengo la Ofisi za Makao Makuu ya TARURA mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kufungua jingo la la Ofisi za Makao Makuu ya TARURA mjini Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Wafanyakazi mbalimbali wa Serikali mara baada ya kufungua jingo la Ofisi za TARURA mkoani Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Tarafa wa Wilaya Mbalimbali ambao walikabidhiwa Pikipiki ili ziweze kuwasaidia katika kazi zao za kila siku.

PICHA NA IKULU

********************************

Na. Frank Mvungi na Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami katika mji wa Serikali utakaogharimu zaidi ya bilioni 89 ikiwa ni ahadi aliyotoa mara baada ya kutangaza Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi ili kutekeleza tamko alilolitoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1973 zaidi ya miongo mine iliyopita.

Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati akiweka jiwe la msingi la mradi huo na baadae kuzindua jengo la Ofisi za Wakala wa barabara Mijini na Vijijini (TARURA) alisema wakala huo umetekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuwataka kuongeza kasi zaidi.

“Ujenzi wa barabara hii utakua na njia nne zenye urefu wa km 11.2, njia mbili zenye urefu wa km 28, njia za waenda kwa miguu, njia za baiskeli na limetengwa eneo la huduma za kijamii,”

“Dodoma ni mji unaokua vizuri, kuna miradi mikubwa iliyokwishatekelezwa na inayotarajiwa kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko ya njia nne yenye urefu wa km 110 itakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni 600 na ujenzi wa Uwanja wa Ndege mkubwa utakaogharimu shilingi bilioni 500” alisisitiza Rais Dkt. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli alitoa tahadhari kwa TARURA kutumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara na sio kuendelea kujenga ofisi zingine katika wilaya mbalimbali nchini na badala yake watumie majengo ya Serikali katika mikoa na wailaya mbalimbali nchini.

Vilevile, Taasisi za Serikali zimetakiwa kujenga majengo yake badala ya kuendelea kulipa pango katika majengo ya kukodi, na ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kumaliza ujenzi wa  jengo lake hapa jijini Dodoma kabla ya mwaka 2020 kumalizika.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) imeidhinisha dola za Marekani milioni 14.3 za msamaha wa kodi ya madeni ambayo nchi ilikuwa ikidaiwa na kutaja sababu ya msamaha huo kuwa nchi imefanikiwa kupambana vizuri dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) unaosababishwa na virusi vya Corona.

“Kwa niaba ya watanzania nitamuandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa IMF kumpongeza kwa kutambua juhudi zetu na fedha hizi tutazitumia vizuri katika kupambana na ugonjwa huu pamoja na kushughulikia mambo mengine yakayosaidia ugonjwa huu usije tena” alisisitiza Rais Magufuli

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekabidhi pikipiki kwa Maafisa Tarafa kwa lengo la kutatua changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiwakwamisha katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali katika maeneo yao.

“Nilitoa kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kununua pikipiki hizi, zimepatikana pikipiki 448 na Maafisa Tarafa  ni 570 nchi nzima, hivyo natumaini hakuna Ofisa Tarafa atakayekuwa hana pikipiki kwani kuna waliogawiwa zamani, watakaoharibu ama kupoteza watazilipa” alisisitiza Rais Magufuli.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa corona, Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Afya kukiendeleza Kitengo cha Tiba Asili kuendelezwa sambamba na kuongeza bajeti yake, na kuwataka wanaotengeneza dawa za asili kutodharauliwa.

“Corona bado haijaisha lakini imepungua sana, hivyo tuendelee kuchukua tahadhari, watu waliodhani tutafariki wengi wameshindwa. Mungu wetu anatupenda na tuendelee kumtegemea yeye” aliongeza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli wakati wa ufunguzi wa jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji amesema kuwa moja ya changamoto zilizokuwa zikilikabili Jeshi hilo ni upandishwaji wa vyeo kwani waliokuwa juu hawakujali wa chini, hali iliyosababisha tuchukue hatua kwa kuwapandisha vyeo Makamanda 889. Tunawahakikishia tutaendelea kuwapandisha kadri itakavyowezekana.

Akizungumzia utendaji wa Jeshi hilo, Rais Magufuli amesema kuwa ameshatoa maagizo kwa Taasisi ya Nyumbu  kushirikiana na Jeshi hili kuanza kutengeneza magari ya zimamoto nchini.

“Kulikuwa na mapendekezo ya Makamishna wanne wa jeshi hili kushushwa vyeo au kufukuzwa kazi lakini kwa kuwa mmefanya marekebisho ya kutosha nimewasamehe, hata aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Jeshi, Thobias Andengenye nimemsamehe lakini nitampangia kazi nyingine,”alisisitiza Rais Magufuli.

Aidha, ametoa wito kwa Viongozi wa Manispaa, Majiji na Wizara ya Ardhi kuhakikisha wanawaelimisha watu kuwa katika kila jengo itengenezwe njia zitakazotumiwa na jeshi hili mara yanapotokea majanga ya moto.

Kwa kutambua umuhimu wa jeshi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Rais ameahidi kuwaunga mkono kwa kuwapa shilingi bilioni 5 ndani ya wiki hii ili kutatua changamoto ya makazi ikizingatiwa tayari jeshi hilo limetafuta eneo la kujenga makazi ya familia 80.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga alimshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwapa kiasi cha shilingi bilioni 2,656,146,300 kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Dodoma.

Aidha, Jeshi hilo  limepata mafanikio katika kukabiliana na matukio ya moto 6,398 na maokozi 2,663 yalishughulikiwa kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 ambapo maeneo 319,389 na vyombo vya moto 17,740 vimekaguliwa ili kuimarisha hali ya usalama wa wananchi na mali zao.