…………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
Mbunge Viti Maalum – Pwani, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema ataendelea kupiga kazi na kutumikia wanawake pamoja na wananchi si kwa ajili ya uchaguzi bali kwakuwa amepewa dhamana ya kutumikia wananchi kipindi cha miaka mitano .
Aliyasema hayo ,wakati alipotoa mchango wa vyerehani 29 katika hatua ya awali kwa kundi la watu wenye Ulemavu kupitia mashirikisho yao ya ngazi za Wilaya na Mkoa.
Mgalu amefanya tukio hilo kwa kuitekeleza Ilani ya CHAMA CHA AMAPINDUZI, Ibara za 50 ‘O’ na 166, ambazo zinatambua Makundi yenye uhitaji maalum ikiwemo; wazee, watoto na watu wenye ulemavu. Chama Cha Mapinduzi kimeweka misingi kuhakikisha watu wenye ulemavu wanalindwa na vitendo vinavyoshusha utu ikiwemo ubaguzi, uonevu, na ukatili.
“Sisi UWT ndio Jumuiya kimbilio ya wanawake, na Katiba ya UWT ndivyo inavyosema,Niliahidi kila Kata itapata vyerehani viwili, ngazi ya Wilaya vyerehani vinne, na Mkoa vyerahani vitano. Vyerehani hivi vitawafikia wote, niwe madarakani au nisiwe madarakani.”alieleza Mgalu
Aidha,Mgalu aliwaahidi watu wenye Ulemavu mkoani Pwani ambao wana sifa za kujiunga na vyuo vya maendeleo ya wananchi kuwapa ufadhili katika masomo yao.
Pia, ameahidi kulipia Kodi ya miezi sita (6) kwa mashirikisho ya watu wenye ulemavu ngazi ya Wilaya, ambapo mahali vyerehani hivyo vitakapowekwa ili kuanza shughuli za ushonaji.
Pamoja na hilo Mgalu alieleza wakati anaingia madarakani alianza na vifaa vya ofisi za kata za UWT ili kuimarisha utendaji kazi na ni wajibu wake hadi hapo kipindi chake kitakapokoma.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa OWM-Walemavu Stella Ikupa, ambaye alikua Mgeni rasmi, alimshukuru Mgalu na kusema ungetoa msaada huu wa vyerehani kwa Jumuiya ya UWT pekee wangesema anatafuta kura, lakini kwa kuwapa watu wenye Ulemavu ni upendo mkubwa.
Mgalu amekuwa akitoa michango mbalimbali kwa Jumuiya, Chama, na wananchi wa Pwani kwa ujumla, hakika anastahili pongezi. Na wananchi wa Pwani wana haki ya kujivunia uongozi wake.
Sambamba na hilo, mwenyekiti wa UWT Pwani Farida Mgomi, na Judith Mruge, kwa niaba ya Chama na Jumuiya walitoa shukurani kwa Mgalu kwa kuwa kiongozi mwenye upendo kwa wananchi wa Pwani, na mwenye kujali majukumu yake akiongozwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kuleta maendeleo chanya mkoani humo.