Wakazi wa kijiji cha Fundimbanga kata ya Matemanga wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma pamoja na Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini Mhandisi Ramo Makan aliyevaa kapelo wakifurahia ujenzi wa darala katika Mto Nanyungu linalojengwa na Wakala wa barabara vijijini na mjini Tarura kwa gharama ya zaidi ya bilioni 1.5 sambamba na ujenzi wa barabara km 5.5 ambayo inakwenda kumaliza changamoto ya wananchi hao kuvuka mto Nanyungu unaotajwa kuwa na wanyama wakali kama Mambo.
Picha na Mpiga Picha Wetu
………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu,Tunduru
WAKAZI wa kijiji cha Fundimbanga kata ya Matemanga wilayani Tunduru, wameipongeza Serikali kwa kujenga daraja la kisasa litakalounganisha kijiji hicho na maeneo mengine ya wilaya ya Tunduru.
Wametoa pongezi hizo jana mbele ya Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini Ramo Makani aliyetembelea kijiji cha Fundimbanga kukagua na kuhamasisha kazi za maendeleo sambamba na kusikiliza kero za wananchi wa kijiji hicho.
Wamesema, kujengwa kwa daraja hilo kutamaliza tishio la wananchi wa kijiji hicho cha Fundimbanga hasa wanafunzi wanaovuka mto Nanyungu kila siku kwenda shule ya sekondari Matemanga kuliwa na mamba pindi wanapovuka mto huo.
Wamesema, baadhi ya wananchi wamepoteza maisha yao kwa kusombwa na maji na wengine kuliwa na mamba,kwa hiyo kujengwa kwa daraja hilo ni ukombozi mkubwa kwa maisha na uchumi wao.
Habiba Linyama na mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho wamesema,kujengwa kwa daraja katika mto Nanyungu ni ishara kuwa Serikali inathamani maisha ya wananchi na kuhaidi kulitumia daraja hilo kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Hata hivyo, wameiomba wakala wa barabara mjini na vijijini Tarura kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ili liweze kutumika kusafirisha mazao na kurahisisha mawasiliano kati ya kijiji cha Fundimbanga na vijiji vya jirani.
Kwa upande wake Mbunge wa JImbo la Tunduru Kaskazini Mhandisi Ramo Makan alisema,Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuri itaendelea kujenga,kuimarisha na kuboresha huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali ndani ya jimbo hilo na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi zinazo fanywa na Serikali yao.
Aidha Ramo amefurahishwa na kazi mzuri ya ujenzi wa daraja hilo lililoharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5 pamoja na matengenezo ya barabara yenye urefu wa km 5.5 ambayo inakwenda kumaliza changamoto ya kuvuka mto Nanyungu ambao ni hatari kwa maisha ya wananchi.
Alisema, serikali ilishawahi kujenga madaraja sita kwa nyakati tofauti ambayo yalisombwa na maji kutokana na kukosekana kwa ubora,kwa hiyo daraja hilo ni la kiwango kikubwa na mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kijiji cha Fundimbanga.
Alisema, mradi huo ulianza kwa kujengwa daraja na kufuatiwa na barabara kutoka eneo la Tabora Pachani hadi kijijini ambapo hadi sasa daraja hilo limekamilika kwa asilimia 98 na sehemu ndogo iliyobaki itakamilika baada ya muda mfupi.
Alisema, barabara hiyo itakuwa kiunganishi kati ya wilaya ya Namtumbo na Songea mkoani humo na mpango uliopo kuifanya barabara hiyo kuwa barabara kuu ambapo mtu anayetoka Matemanga atapita barabara hiyo kwenda hadi Nalasi badala ya kulazimika kwenda Tunduru mjini.
Amewahimiza wananchi wa kijiji cha Fundimbanga na kata yote ya Matemanga kuitumia barabara hiyo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuitumia kukuza uchumi wa familia zao.
Alisema, kujengwa kwa daraja na barabara hiyo ni sehemu ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambapo wananchi wa kijiji hicho walikipa ridhaa chama hicho kuunda Serikali iliyopo madarakani na serikali kwa kutambua umuhimu wa wananchi hao ndiyo maana imeamua kuboresha miundombinu hiyo pamoja na huduma nyingine za kijamii.