Mfanyabiashara wa Nafaka wa eneo la Tabata Jijini Dar es Salaam akitoa maoni yake kwa Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Lameck Ndinda wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea mkoani Dar es Salaam.
PICHA ZOTE NA TRA.
Wafanyabiashara wa Tabata jijini Dar es Salaam wameishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi na kusema kuwa, elimu hiyo itawasaidia kuongeza uhiari wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Wakizungumza wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayofanyika jijini hapa, wafanyabiashara hao wamesema kwamba kitendo cha TRA kuwatembelea katika maduka yao na kutoa elimu ya kodi kutaongeza ari ya kulipa kodi kwa wakati na kupunguza idadi ya wakwepa kodi ambao baadhi yao hawajui umuhimu wa kodi.
“Kazi wanayoifanya TRA ya kuwaelimisha wafanyabiashara katika maduka yao ni nzuri mno kwa sababu hata wale wasiojua umuhimu wa kulipa kodi nao watajua faida ya kodi na hawatakuwa na kisingizio tena cha kudai kuwa hawana elimu ya kodi na hivyo watalipa kodi zao kwa wakati,” alisema Bento Bidyanguze ambaye ni mhasibu wa baa ya Nyantare iliyopo Tabata Bima jijini Dar es Salaam.
Naye Mfanyabiashara wa spea za pikipiki wa Tabata relini Bw. Donath Munishi aliishukuru TRA kwa kumpatia elimu ya kodi na kuomba zoezi hilo liwe endelevu kutokana na umuhimu wake kwa wafanyabiashara.
“Kwakweli ninaishukuru TRA kwa kunielimisha mambo mbalimbali yanayohusu kodi lakini naomba elimu hii itolewe mara kwa mara maana sote tunajua elimu haina mwisho hivyo TRA wasichoke kututembelea na kutuelimisha ili kutukumbusha wajibu wetu wa kulipa kodi kwa wakati”, alisema Munishi.
Kwa upande wake Bi. Rehema Seboha ambaye ni mfanyabiashara wa vitambaa vya kutengenezea sofa kutoka Tabata relini, ametoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuwapokea maafisa wa TRA na kuwasikiliza ili waweze kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu kodi kwa ajili ya ustawi wa biashara zao.
“Mimi binafsi nimefurahi sana kutembelewa na maafisa wa TRA ambao wamenielimisha kwa kina kuhusu utunzaji wa kumbukumbu za biashara yangu pamoja na kulipa kodi kwa wakati hivyo nawasihi wafanyabiashara wenzangu wawapokee maafisa hawa ili na wao wanufaike na elimu hii ya kodi kwa faida yao wenyewe,” alisema Bi. Seboha.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayofanyika jijini Dar es Salaam imeanza tarehe 8 na itamalizika tarehe 12 Juni, 2020 ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya kodi, kusikiliza maoni, kero na changamoto za wafanyabiashara na kuzitafutia ufumbuzi.