Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akisisitiza jambo katika Mkutano uliyohudhuriwa na wanunuzi wa zao la zabibu na shahiri pamoja na wakulima wa mazao leo jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki katika Mkutano uliyohudhuriwa na wanunuzi wa zao la zabibu na shahiri pamoja na wakulima wa mazao leo jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo katika Mkutano wa wanunuzi wa zao la zabibu na shahiri pamoja na wakulima wa mazao hayo ili kuleta malengo chanya.
Baadhi ya wajumbe katika Mkutano uliyohudhuriwa na wanunuzi wa zao la zabibu na shahiri pamoja na wakulima wa mazao hayo wakimsikiliza Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (hayupo pichani).
………………………………………………………………………………
Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
Serikali imekutana na wadau wa zao la shahiri na zabibu kwa lengo la kurejesha zao la shahiri na kutatua changamoto zilizopo katika sekta ndogo ya Zabibu ili kuweza kukuza soko la mazao hayo na kuinua kipato cha wakulima wake.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe katika Mkutano uliyohudhuriwa na wanunuzi wa zao la zabibu na shahiri pamoja na wakulima wa mazao hayo.
Aidha Mhe. Bashe amesema kuwa kwa sasa wakulima wa shahiri hawana soko, hivyo ni vyema kwa msimu ujao wakulima walime zao la shahiri.
Mhe. Bashe ameuagiza uongozi wa kiwanda cha Tanzania Breweries (TBL) kufunguliwaa au kukikodisha kiwanda cha Kilimanjaro ambacho kipo mikononi mwao ili kianze kazi mara moja.
“Lengo ni kutaka wakulima waweze kulima kwa msimu ujao na sisi serikali tutahakikisha mikataba inakuwa sawa kwa pande zote mbili kwa mnunuzi na mkulima na uwazi wa mikataba hiyo ili kila mmoja kunufahika katika zao hilo”, ameeleza Mhe. Bashe.
Hata hivyo katika mkutano huo Mhe. Bashe amewataka wakuu wa wilaya, wakuu wa mkoa na warajis wa vyama vya ushirika watakapo saini mikataba hiyo na Serikali ishirikishwe kikamirifu ili kulinda maslahi ya mkulima na wanunuzi.
Kwa zao la zabibu Mhe.Bashe amesema msimu wa kilimo unaanza mwezi wa nane hivyo Serikali inahitaji uhakika wa masoko na wanunuzi wanatakiwa kusema namna ambavyo watanunua zao la zabibu .
“Hatutaki wakulima wa zabibu mwezi wa nane wakati wa kuvuna wapate shida ya masoko na nahitaji kujua kwa mwezi huo tutavuna kiasi gani . Njia pekee itakayotusaidia ni kuingia mkataba na wakulima” ameweka wazi Mhe. Bashe.
Kwa kuongezea Mhe. Bashe ametoa wito kwa wakulima kutotegemea zao moja bali wajikite pia kwenye mazao mengine na kuwataka kampuni ya wanunuzi kununua shahiri kwa wakulima wote .
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi.Theresia Mahongo amesema zao hili ni zao la kibiashara linalowaingizia uchumi wakulima hivyo ametoa rai kwa wanunuzi kuongeza tani kwa zao la shahiri kwani wakulima wanalima zaidi ya tani 8,000 zinazohitajika
Mkurugenzi wa Tanzania Bruweries (TBL) Bw.Philip Redman amesema kwa msimu ujao wa 2021,wameingia mkataba na wakulima 300 na kiwanda kina uwezo wa kuchukua tani 5,000 kwa mwaka.
Kwa upande wa Serengeti Breweries (SBL) Mkurugenzi wa Mahusiano Bw.John Wanyancha amesema kuwa kwa msimu ujao wanatarajia kuchukua tani 3,000 kwa wakulima 60.
Huku Mkulima wa shahiri Bw. Domisiani William kutoka Karatu ameeleza changamoto wanazokumbana nazo ni mapato na bei ndogo ya zao hilo pia ameiomba Serikali kuongeza tani kwani wakulima wanalima zaidi.