Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala (wa tatu kutoka kulia) akiongoza maelfu ya Watanzania katika ibada maalum ya kuuaga ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) iliyofanyika katika Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania iliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro.
Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Ararm Mwantyala akiongoza maelfu ya Watanzania katika maombi ya kumshukuru Mungu kwa kuiondoa corona nchini Tanzania. (Picha na Sauti ya Uponyaji Tanzania).
……………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Kihonda
MAELFU ya Watanzania wameungana katika Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania iliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro kuuaga rasmi ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19).
Akiongoza ibada hiyo, Kiongozi Mkuu wa huduma hiyo, Nabii Joshua Aram Mwantyala amesema, Mungu amejibu maombi ya Watanzania yaliyohamasishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt.John Magufuli kwa kila mmoja kumuomba Mungu ili aweze kuuondoa ugonjwa huo katika Taifa letu.
“Mungu ni mwingi wa rehema na hakuna jambo lisilowezekana kwake, kwani baada ya kujinyenyekesha mbele zake,kuonyesha kuwa yeye ni Mungu wetu, kuonyesha kuwa vyote viko mikononi mwake na tukampa heshima kuu, hakika amesikia maombi yetu Watanzania, sasa Dunia inaendelea kujihoji maswali lukuki, juu ya huu ukuu wa Mungu kwa Taifa letu, hakika tutaendelea kumtukuza yeye daima,”amesema Nabii Joshua.
Amesema, kupitia ibada hiyo ya kumshukuru Mungu pia iliwajumuisha watu kutoka mataifa ya nje ambao anaamini wataenda kuueleza ulimwengu juu ya matendo makuu ambayo Mungu anayafanya kwa Tanzania.
“Biblia Takatifu kitabu cha Yakobo 5: 15-16 kinaeleza wazi kuwa, kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana akiomba kwa bidii, nasi hatutaishia hapa tu, tutaendelea kumuombea Rais wetu mheshimiwa Dkt.John Magufuli, wasaidizi wake na Watanzania wote ili azidi kuyatenda mambo makuu kwa Taifa letu la Tanzania,kila mmoja wetu ni shaidi.
“Mheshimiwa Rais ni miongoni mwa marais wachache duniani ambao, Mungu ndiye kimbilio lao iwe katika tabu na raha,haya ni mafanikio makubwa mno,hivyo kupitia uongozi wake uliotukuka, Mungu ametushindia mapito magumu ambayo yanawatesa watu huko duniani,”amesema Nabii Joshua.
Wakati huo huo, Nabii Joshua amewataka Watanzania kuendelea kutengeneza mahusinao mema na Mungu kila saa kwa kuwa, hiyo ni njia rahisi ya kuwasilisha mahitaji muda wowote na yakajibiwa kwa wakati.
“Maandiko kupitia Biblia Takatifu yanaeleza wazi kuwa, haja zenu na zijulikane mbele za Mungu, hii inamaanisha kuwa, licha ya Mungu kuzijua haja zetu,lakini bado anahitaji tumuombe tena kwa bidii.
“Pia tutambue, Mungu haitaji kujua hali yako ikoje muda huu bali anahitaji kujua unataka nini, taswira au picha ya tatizo lako unatakiwa uwe nayo mwenyewe, lakini mbele za Mungu unatakiwa upeleke haja ya moyo wako na si malalamiko, ndiyo mana maombi haya ya kuidhibiti COVID-19 Mungu alijibu mapema, maana alijua haja ya mioyo yetu Watanzania ni kuondolewa hilo tatizo,”amesema Nabii Joshua.