katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akizungumzia umuhimu wa kuhifadhi michoro inayopatikana katika eneo la Saiti 3B na maeneo mengine kwa Mkuu wa Kituo cha Michoro ya Miambani cha Kolo Kondoa Bw. Zuberi Mabie (kulia) wakati alipotembelea kituo cha Michoro ya Miambani kilichopo Kolo Kondoa mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda akionesha Mchoro wa Tembo uliochorwa katika Saiti 2B na jamii ya kale iliyokua ikiishi maeneo hayo enz. za kale, wakati alipotembelea Kituo cha Michoro ya Miambani cha Kolo Kondoa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda (katikati) akisoma kibao kinachotoa maelezo kuhusu Michoro ya Miambani wakati alipotembelea kituo cha Michoro ya Miambani cha Kolo Kondoa, kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Malikale Bw. Revocatus Bugumba na kushoto kwake ni Bw. Zuberi Mabie ambaye ndiye Mkuu wa Kituo hicho.
……………………………………………………………………………………….
Na John Bera,Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda ametembelea kituo cha Michoro ya Miambani cha Kolo kilichopo eneo la malikale wilayani Kondoa Mkoani Dodoma lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa eneo hilo linatunzwa vizuri kwani ni miongoni mwa sehemu ambazo zina vivutio vikubwa kwa watalii.
Akizungumza mara tu baada ya kutembelea kituo hicho cha Michoro ya Miambani cha Kolo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda amesema, eneo hilo ni sehemu ya Utalii wa Ndani na litasaidia kuvutia zaidi watalii wanaokuja hapa nchini.
“Eneo hili ni eneo zuri kwa Utalii wa Ndani, kwani lipo karibu sana na jiji la Dodoma pia ni rahisi kufika hapa, tukimaliza kutengeneza kituo kizuri cha kupokea wageni hapa watu wanaweza kuja, wakaleta watoto ili wajue kwamba babu zetu walifanya nini zamani ” amesema Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda amesema kuwa, tukiweza kuweka miundombinu vizuri, tunaweza kuvutia watalii wengi zaidi huku akiwasisitisa watanzania kuona umuhimu wa kujivunia vivutio walivyo navyo hapa nchini.
” Wageni wa kimataifa walikodisha ndege kwaajili ya kutembelea eneo hili kutoka Arusha na kuja hapa lengo lao lilikuwa ni kuja kuangalia Michoro ya Miambani “
Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda amesema, serikali inataka utalii usibaki tu katika nyanja moja ya kwenda kuangalia wanyamapori au kwenda kupanda mlima Kilimanjaro, bali uwe wa kuangalia ustarabu wa zamani kwani eneo la Malikale bado halijatumiwa sana.
” Tunayo kondoa, kuna Kilwa kuna urithi mkubwa sana, kuna michoro Musoma ambayo bado tunaihitaji kuihifadhi, kuna Iringa na watu dunia nzima wanapenda kuja kuangalia michoro hii ambayo, inaonesha kuwa, yalikuwa makazi ya babu zetu wakati huo walipo kuwa wakija kupumzika katika maeneo hayo” Amesema Prof Mkenda.
Sanjari na hayo ametoa wito kwa vyuo vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es salam, ambacho kina idara nzuri ya Akiolojia na vyuo vingine kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuwapeleka wanafunzi na watafiti wengine kwenda kufanya utafiti wa kitaalamu kwenye eneo hilo.
Kwa upande wake Zuberi Mabie ambaye ni Mkuu wa kituo cha Michoro ya Miambani cha Kolo kilichopo Kondoa amesema, eneo hilo ni sehemu ambayo ina michoro ya kale ambayo ilikuwa ikichorwa na mababu zetu kwani kabla ya kugundulika kwa maandishi, mwanadamu aliweka kumbukumbu zake kupitia uchoraji katika maeneo ambayo yana miamba.
“Mwanadamu amepitia hatua mbalimbali za namna ya kutunza kumbukumbu leo hii tuna mifumo mbalimbali kama kutumia kompyuta lakini wao zamani walitumia kuweka kumbukumbu zao kupitia sanaa ya uchoraji “
Sanjari na hayo amesema kama ilivyo maeneo mengine ya dunia , Michoro ya Kondoa Irangi kwa kanda ya Afrika mashariki inaonekana kuwa ndiyo michoro ya kale zaidi katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Hata hivyo Prof. Mkenda amesema, kwa Tanzania kituo cha Kolo, ndicho sehemu yenye michoro mingi zaidi kwani wakati huo ilichorwa na jamii ya wawindaji ,waokota matunda, wakulima na wafugaji.