Muonekano wa Kituo cha kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha serikali (TANOIL)kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, kilichofunguliwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Juni 06, 2020 wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani( wa tatu kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said( kushoto), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( pili kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima( katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC) Dkt. James Mataragio (wa tatu kulia) na Viongozi wa Waandamizi wa Wizara ya Nishati na taasisi zake, Viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Mara wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali( TANOIL) kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANCOIL, kilichofunguliwa na Waziri huyo , Juni 06, 2020 wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata sili katika gari iliyobeba mafuta, ili kufungua koki kuruhusu mafuta kuingia katika matanki ya kuhifadhi mafuta ya kituo cha kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha TANCOIL,alipozindua rasmi biashara ya mafuta katika kituo hicho kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANCOIL, kilichofunguliwa na Waziri huyo , Juni 06, 2020 wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake, Viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Mara baada ya ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali( TANOIL) kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANCOIL, kilichofunguliwa na Waziri huyo , Juni 06, 2020 wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati akifungua rasmi biashara ya mafuta katika kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali(TANOIL) kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Juni 06, 2020, wilayani Musoma mkoani Mara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC), Dkt. James Mataragio akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali kitakachosimamiwa na TPDC kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho, Juni 06 ,2020, wilayani Musoma mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Nishati , Subira Mgalu akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali kitakachosimamiwa na TPDC kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho, Juni 06 ,2020, wilayani Musoma mkoani Mara.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Mara wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali kitakachosimamiwa na TPDC kupitia Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho, Juni 06 ,2020, wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya TANOIL, ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba wakiteta jambo wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali(TANOIL) kitakachosimamiwa na TPDC, Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho Juni 06, 2020, wilayani Musoma mkoani Mara.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima wakielezana jambo wakati wa ufunguzi wa kituo cha kuuza mafuta ya Dizeli na Petroli cha serikali(TANOIL) kitakachosimamiwa na TPDC, Dkt. Kalemani alifungua kituo hicho Juni 06, 2020, wilayani Musoma mkoani Mara.
………………………………………………………………………………………..
- Dkt. Kalemani afungua Kituo cha kwanza Mara, TPDC kujenga vituo 100.
Na Zuena Msuya, Mara
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi biashara ya kuuza na kusambaza mafuta nchini kwa kufungua kituo cha kwanza kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha Serikali kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kupitia Kampuni yake Tanzu ya Mafuta ( TANCOIL).
Aidha Dkt. Kalemani alisema kuwa kuzinduliwa na kufunguliwa kwa biashara hiyo ni kutimiza azma na nia njema ya Serikali ya kuboresha shirika lake la TPDC,kuwapatia na kuwasogezea karibu wananchi wake huduma ya kupata mafuta yenye viwango vya ubora unaotakiwa, bei nafuu, na yatakayopatikana kwa wingi muda wote.
Dkt. Kalemani alifanya Uzinduzi huo pamoja na kufungua kituo hicho wilayani Musoma, mkoani Mara Juni 6, 2020, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa huo, akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara hiyo na Taasisi zilizochini yake.
Alisema baada ya kuanza rasmi kwa biashara hiyo, TPDC kupitia TANCOIL itashirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanikisha azma ya Serikali ya kufungua na kuweka vituo vya kuuza na kusambaza mafuta katika kila halmashauri nchini pamoja na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.
“Tumeshaanza biashara ya kuwauzia wananchi wetu mafuta, sitegemei kusikia mafuta yanauzwa kwa bei aghali katika vituo vya serikali, TPDC na TANCOIL mnielewe vizuri hapa! hii haipo na haitakuwepo, lengo letu sisi serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wapata bidhaa bora za mafuta kwa kiwango kinachotakiwa, kwa bei nafuu na yatapatikana kwa wingi wakati wote na huduma hii inapatikani jirani na maeneo yao!,”Alisema Dkt. Kalemani.
Dkt. Kalemani aliwaeleza watanzania kuwa TPDC na TANOIL watashiriki katika biashara ya uagizaji na usambazaji mafuta kama zinavyofanya kampuni zingine za mafuta nchini ili kuongeza ushindani na kutanua wigo wa kampuni za kizalendo kushiriki katika biashara ya mafuta, ambayo kwa sasa inafanywa na makampuni kutoka nje ya nchi tu.
Alisema kuwa serikali kupitia TPDC itajenga vituo 100 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kutenga maeneo yatakayojengwa vituo hivyo: Aidha itahakikisha kuwa nusu ya mafuta yote yanayoingizwa nchini yanasimamiwa TPDC.
“Watanzania tutembee kufua mbele na kujivunia vilivyo vya kwetu! Uzinduzi wa biashara hii ya mafuta hapa Musoma leo unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ya Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli, ni kutambua juhudi na mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kuimarisha sekta ya Umma ya kukuza uchumi, pia hatuna budi kutambua mchango wake wa kuanzisha TPDC mwaka 1969 pamoja na kiwanda cha kusafisha mafuta cha TIPER mwaka huohuo, ambapo TPDC ilimiliki kiwanda hicho kwa asilimia 50%, mwalimu aliona na kuwaza mbali sana, hii yote ni katika dhana ya kujitegemea kiuchumi,”. Alisisitiza Dkt. Kalemani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini, (TPDC), Dkt. James Mataragio alisema kuwa katika kutekeleza azma hiyo ya serikali, kuanzia mwaka huu wa fedha 2020/2021, TPDC imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya mtaji wa kugharamia shughuli za uagizaji, usambazaji na usimamizi wa mauzo ya mafuta nchini kote.
Dkt. Matagio, alisema kwamba TANOIL imejipanga kuhakikisha kuwa, kunakua na usalama wa usambazaji mafuta nchini yaani (security of supply), kunapatikana takwimu sahihi za mafuta, bei na viwango stahiki vya ubora, pamoja na uelewa mzuri na mpana wa biashara ya mafuta nchini.
“Ninafuraha sana leo TPDC inaandika historia mpya na kubwa sana katika nchi yetu, tunaungana na wakazi wa Mkoa wa Mara, kwa niaba ya watanzania wote kuonyesha furaha yetu katika kuandika historia hii mpya ya kwamba shirika letu na maendeleo ya Mafuta, (TPDC) linarudi kwa kishindo katika biashara ya kuuza na kusambaza wa mafuta ya Petroli, Dizeli na bidhaa zake kwa maslahi yetu sote na taifa kwa ujumla”, Alisema Dkt. Mataragio.
Alieleza zaidi kuwa Mwaka 2000, Serikali ilifanya maamuzi ya kuendesha biashara ya mafuta nchini kwa mfumo wa soko huria, hivyo TPDC ikaunda kampuni tanzu ya COPEC kuweza kuingia katika mfumo huo na kushiriki katika soko la ushindani katika biashara hiyo.
TPDC ilinunua na kujenga vituo mbali mbali nchini vikiwemo Segera na Muheza Mkoani Tanga, Makuyuni na Makumira Mkoani Arusha, Singida, Geita, pamoja Mkoani Mara ambapo vilinunuliwa vituo viwili tu cha Musoma na Tarime, vituo vyote hivyo vinamilikiwa na TPDC kwa asilimia mia moja(100% ).
Dkt. alisema kuwa TPDC ilishiriki katika biashara hiyo kupitia katika vituo hivyo,hata hivyo kukosekana kwa Sheria madhubuti ya Mafuta/Petroli, kulififisha ushiriki wa TPDC katika soko lenye ushindani mkubwa.
Aliweka wazi kuwa baada ya kufanyika kwa michakato na mapitio ya rejea , maboresho mbalimbali ya shirika hilo pamoja na mambo mengine, kumewezesha Uwepo wa Sheria madhubuti, pamoja na usimamizi wa kanuni mbalimbali, ambazo sasa unaiwezesha TPDC kuingia katika soko kwa ufanisi zaidi.
Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 imeipa TPDC hadhi ya kuwa Shirika la Mafuta la Taifa (NOC) ili kujiendesha kibiashara, kupitia Sheria hiyo, TPDC imeimarisha kampuni zake Tanzu za GASCO na TANOIL. Awali, TANOIL ilikuwa COPEC. Kampuni ya GASCO inajishughulisha na biashara ya gesi na TANOIL inajishughulisha na biashara ya mafuta, ambayo ndiyo biashara tunayoizindua leo Kitaifa.
Katika mwaka huu wa fedha, TPDC itakamilisha ujenzi wa vituo viwili katika Mkoa wa Singida na Mkoa wa Geita. Aidha, TPDC inaendelea na mkakati wa kutwaa ardhi katika mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Dodoma na Morogoro. Hatua za utwaaji ardhi katika mikoa ya Dodoma na Tanga zipo katika hatua za ukamilishaji.
“Natumia fursa hii kwa niaba ya TPDC kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati unayoiongoza wewe Dkt. Kalemani kwa umahiri, kwa maelekezo na rasilimali fedha zinazoiwezesha TPDC sasa kuingia katika biashara hii, pia Serikali ya Mkoa wa Mara kwa ushirikiano waliotupatia kwa muda wote tangu enzi za COPEC hadi sasa tunapokuwa TANOIL na kufungua ukurasa mpya wa mafanikio ya uzinduzi wa biashara ya mafuta”, Alisema Dkt. Mataragio.
Naye Mkuu wa Mkoa, Adam Malima, aliwaasa wakazi wa wafanyabiashara na watumia wa mafuta ya Petroli na Dizeli kuunga mkono juhudi za serikali za kuanzisha bishara ya mafuta kwa kununua mafuta katika vituo vya serikali.
Sambamba hilo alisema kuwa kutokana mikakati iliyowekwa na serikali kupitia TPDC na TANOIL kufikisha huduma ya mafuta hayo karibu na wananchi,kutaweka katika mazingiza salama na rafiki watumiaji wa mafuta hayo hasa waendesha bodaboda na wafanyabiashara wadogo.
“Wafanyabiashara wadogo wanaowauzia waendesha bodabora na vyombo vingine vidogo vinavyotumia mafuta hayo, wamekuwa wakihifadhi bidhaa hiyo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha na mali zao, wanatumia vifungashio duni kama Galoni na chupa za maji, kiukweli hii itaondoa kabisa hatari hii iliyopo katika jamii yetu hasa vijijini”, Alisema Malima.
Historia inatuonesha kwamba katika miaka ya 80 hadi kufikia Mwaka 2000, TPDC licha ya biashara yake kuu ya utafutaji, uchimbaji, uendelezaji na usambazaji wa gesi asilia ilikuwa muagizaji, muingizaji na msambazaji mkuu wa mafuta yote yaliyotumika nchini.
TPDC iliingiza mafuta ghafi nchini na kuyasafisha, na pia uingizaji wa ziada ya mafuta yaliyosafishwa na kutosheleza mahitaji ya mafuta nchini.
Pia TPDC ilibeba jukumu hilo kwa ufanisi na uzalendo wa hali ya juu, ikiwemo kuwa msambazaji pekee aliyesambaza mafuta mstari wa mbele wakati wa vita vya Kagera kati ya Mwaka 1977/78 baada ya makampuni ya binafsi kugoma kupeleka mafuta Kagera.