**************************
Na Mbaraka Kambona, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mkakati madhubuti wa kutokomeza Magonjwa yanayoandama mifugo ili kuwa na mifugo bora itakayozalisha kwa tija na kukuza uchumi wa nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Tanzania, Profesa Hezron Nonga katika Mkutano wa 45 wa Baraza la Veterinari uliofanyika jijini Dodoma Juni 4,
2020.
Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo, Profesa Nonga alisema kuwa Tanzania kuna mifugo takriban milioni 34 lakini pamoja na wingi huo wa mifugo bado nchi haijafikia uzalishaji mkubwa kutokana na magonjwa yanayoandama mifugo hiyo.
Kufuatia hali hiyo, alisema kuwa Mwaka 2018 Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliamua kuja na mkakati wa kufanya mageuzi makubwa katika huduma za mifugo upande wa afya ili kuwa na mifugo bora itakayotoa mazao bora na salama kwa matumizi ya binadamu.
Profesa Nonga alisema mkakati huo ambao umejikita zaidi katika kukinga mifugo dhidi ya magonjwa umeweka utaratibu wa kuhakikisha mifugo yote inaogeshwa na kupata chanjo stahiki dhidi ya magonjwa ya kipaumbele.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo magonjwa yanayochangia kukwamisha uzalishaji wenye tija kwa mifugo nchini ni ugonjwa wa miguu na midomo, Ndiganakali na mapele ngozi.
“Lengo letu ni kuhakikisha mifugo yote nchini inapata chanjo kulingana na kalenda ya uchanjaji ili kuwakinga na magonjwa hayo sumbufu”, alisema Profesa Nonga.
Aidha, alisema mkakati huo umepanga kuwa katika kila Kijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa kuwe na Majosho ya kuogeshea ng’ombe na mifugo mingine walau mara mbili kwa mwaka ili kuwalinda na maradhi yanayosababishwa na Kupe pamoja na wadudu wengine.
“Kwa mfano Kupe anachangia vifo vya Ng’ombe kwa zaidi ya asilimia 70, hivyo ni muhimu kuzuia magonjwa yanayosababishwa na wadudu hawa ili tuwe na ufugaji wenye tija zaidi nchini, maana ufugaji unakuwa hauna tija pale ambapo wanazaliwa Ndama kumi halafu
wanakufa tisa unabaki na mmoja”alifafanua Mkurugenzi huyo.
Katika kuhakikisha suala la kuogesha mifugo linafanikiwa, alisema kwa mwaka huu wa fedha wa 2019/2020 Serikali imeshajenga majosho 85 na kukarabati majosho 288 na
kusisitiza hawataki kuona mifugo inaendelea kufa wakati wataalamu wapo.
Pia alisema mkakati huo umeweka utaratibu mzuri wa ununuzi wa pamoja wa chanjo (bulk procurement system) na zitasambazwa katika maeneo yote kuanzia ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya mkoa ili ziwe zinapatikana kwa urahisi.
“Utaratibu huu wa ununuzi wa pamoja unatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi wa saba mwaka huu ambapo chanjo zote zitapatikana kuanzia ngazi ya kijiji mpaka mkoani”,
alisisitiza.
Akifafanua hoja ya baadhi ya wafugaji wanaolalamika kuwa chanjo zimekuwa zikiuzwa kwa bei kubwa, Alisema kuwa chanjo ni huduma sio biashara na ndio maana serikali katika mkakati huu imeweka bei ndogo ya chanjo hizo ili kila mfugaji aweze kununua, huku akitolea mfano bei ya chanjo ya homa ya mapafu ya ng’ombe ambayo ni shilingi 550.
“Nia ya Serikali ni kumsaidia mfugaji kuwa na mifugo yenye afya bora ambayo itatoa mazao bora na salama kwa mtumiaji, unaweza kuona kwa mfano Ng’ombe mwenye gharama kubwa Serikali imefanya chanjo yake ipatikane kwa shilingi 550 tu, hivyo ni matarajio yetu wafugaji
watachangamkia fursa hiyo”, alifafanua.
Katika hatua nyingine Profesa Nonga alisema suala la uogeshaji wa mifugo ni la lazima, Serikali imetunga sheria ya uogeshaji na matumizi ya dawa za kuogeshea ya mwaka 2020 ambayo inawataka wafugaji kuogesha mifugo yao.
“Sheria hii inamlazimisha mfugaji kuogesha mifugo yake walau mara mbili kwa mwaka kinyume na hapo ni kosa na adhabu yake ni kulipa kiasi cha shilingi milioni kumi kama faini au jela mwaka mmoja au vyote kwa pamoja kutegemeana na kosa lenyewe” alisisitiza
Profesa Nonga.
Alisema kuwa Serikali inanunua dawa na kuzigawa bure katika majosho na mfugaji atachangia shilingi hamsini (50) kwa kila mchovyo mmoja ikiwa ni kama mchango wa
uendeshaji.
Alitoa wito kwa wafugaji wote kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya awamu ya tano kwa kuhakikisha wanakuwa na mifugo bora itakayozalisha malighafi zitakazoenda viwandani kwa wingi na kwa ubora unaohitajika ili kukuza uchumi wa viwanda.