Home Siasa CCM BAGAMOYO KUKAA MEZA MOJA NA VIONGOZI WA HALMASHAURI YA MJI MDOGO...

CCM BAGAMOYO KUKAA MEZA MOJA NA VIONGOZI WA HALMASHAURI YA MJI MDOGO NA WILAYA

0

****************************

NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kimejipanga ,kuwakutanisha viongozi wa Halmashauri ya Mji Mdogo na wa Halmashauri ya Wilaya, ili kuhakikisha wanashirikiana na kuondoa muingiliano wa mambo kwa maslahi ya wananchi.
Hatua hiyo inalenga kila Mamlaka kutimiza majukumu kulingana na mipaka yake, lengo kubwa ni kuondoa muingiliano wa kazi, hali inayoonekana kujitokeza ikichangia kukwama kwa baadhi ya shughuli za kimaendeleo kwa wananchi.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa CCM wilayani hapo, Abdul Sharifu, akizungumza katika kikao Maalumu kilichoitishwa na Kamati ya Mamlaka ya Mji huo.
Kauli ya Sharifu imefuatia taarifa ya mwenyekiti wa kamati Mpwimbwi aliyoitoa , kwa niaba ya Kamati yake iliyoelezea changamoto ya kutopatiwa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake, ikiwemo kusimamia usafi hali inayosababisha kukwama kwa shughuli za kimaendeleo.
Sharifu alisema kuwa chama kumeguswa na hali ya kutokuwepo kwa ushirikiano kati ya Mamlaka hizo mbili, huku akipongeza uongozi wa Mji kwa kikao kilicholenga kupata suluhu, huku akieleza kuwa kila Mamlaka inapaswa kusimamia upande wake wa kuendeleza ustawi wa wana- Bagamoyo.
“Kwanza nikupongeze Mwenyekiti na Kamati yako, kwa kutukutanisha hapa na kuleta changamoto zinazowakabilia kuhusiana na shughuli zenu za kisheria, tutawakutanisha hapahapa tukishirikisha pande tatu, sisi chama, Mkuu wa Wilaya na ofisi ya Mkurugenzi, ili kuweka mambo sawa” alisema Sharifu.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Salumu Mtelela alipongeza jambo hilo lililofikishwa mbele yao, ambapo alisema wao ndio wasimamizi wa Serikali, na ni sehemu sahihi na kuwa wamepokea changamoto hizo na kwamba watandaa siku watayowakutanisha viongozi wa pande hizo ili kupatikana kwa suluhu.
“Jambo ili kulileta hapa mmefanya kitu sahihi sana, masuala kama haya yanayohusiana na Mamlaka ambazo zimetokana na chama chetu, ni vema yakaletwa kwenye uongozi kuliko nje ya hapa, tunaimani kubwa na Serikali yetu wilayani hapa, chini ya Mkuu wa Wilaya Zainab Kawawa tutashirikiana kuliweka sawa,” alisema Mtelela.
Taarifa ya Mamlaka hiyo iliyosomwa na Mpwimbwi, imeelezea baadhi ya changamoto huku ikitaja mafanikio ya kupata gari kutoka kwa marafiki zao, lakini hakuna msukumo kutoka Halmashauri, kwani gari hilo lina miezi zaidi ya miwili halijaanza kufanyakazi husika.
“Tuliwasiliana na rafiki zetu waliotupatia gari la takataka, lakini tangu liwasili hapa Bagamoyo bado halijaanzakazi, jambo ambalo halileti sura nzuri kwa wahisani wanaoguswa na maendeleo yetu, jambo ambalo linawezaa kuwavunja moyo watu wenye nia ya kutusaidia wana-Bagamoyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.