Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akisoma hotuba kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 5, 2020 jijini Dodoma yaliyoambatana na ufungaji na utoaji vyeti kwa wakaguzi wa mazingira kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Dodoma. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Tutunze Mazingira: Tukabiliane na Mabadiliko ya Tabianchi”. Wengine pichani kulia ni Katibu Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Joseph Malongo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Azzan Zungu akizungumza na washiriki wa mafunzo ya Wakaguzi wa Mazingira katika Siku ya Mazingira Duniani leo tarehe 05 Juni 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akitoa cheti cha kuhitimu mafunzo ya wakaguzi wa mazingira kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoa wa Dodoma kwa Afisa Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Theodory
Mulokozi wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 5, 2020 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Joseph Malongo akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 05, 2020 katika ukumbi wa LAPF Dodoma.
Sehemu ya Maafisa Mazingira kutoka Wilaya na Halmashauri za Jiji la Dodoma ambao leo wamepewa Vitambulisho rasmi vya wakaguzi wa Mazingira baada ya kuhitimu mafunzo ya Siku tatu jijini Dodoma. Mafunzo haya yameandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
*********************************
Na Lulu Mussa
Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema suala la mabadiliko ya tabianchi halitambui mipaka ya kijiografia wala ya kisiasa, hivyo, juhudi za kukabiliana na changamoto hii zinahitaji ushirikiano wa pamoja baina ya Jumuiya za Kimataifa.
Hayo ameyasema hii leo Jijini Dodoma katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani ambapo ameitaka jamii ya watanzania kuendelea kulinda mazingira kwa mustakabali
wa maendeleo endelevu.
Amebainisha kuwa nchi yetu ni Mwanachama wa Jumuiya za Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira za kikanda na za Kidunia, hivyo inatekeleza Sera na Sheria za mazingira
kuendana na makubaliano na maazimio yanayofikiwa katika Jumuiya hizo kwa kadri inavyowezekana.
“Nchi yetu ni Mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi unaojulikana kama Mkataba wa kulinda mazingira wa Paris (Paris Agreement). Katika kutekeleza Mkataba huu, Nchi wanachama zimekubaliana kupunguza uzalishaji wa gesijoto kwa pamoja na kuongeza juhudi za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi” Zungu alisisitiza.
Amesema kuwa Tanzania imeandaa miradi ya kimkakati kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa gesijoto ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) na
ujenzi wa bwawa la uzalishaji wa umeme wa megawati 2115 (Mwalimu Nyerere Hydropower – Stieglers Gorge).
“Malori na mabasi hutumia dizeli ambayo huzalisha gesijoto aina ya hewa ukaa. Reli ya kisasa inayojengwa haitatumia dizeli bali itatumia umeme ambao unatokana na nguvu ya maji, pia kwa kujenga bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere tutaongeza kiasi kikubwa cha umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maji, na kupunguza kwa kiasi
kikubwa matumizi ya gesi asilia na dizeli katika uzalishaji wa umeme” Zungu alisisitiza.
Amebainisha kuwa umeme wa uhakika utakaozalishwa na Bwawa la Mwalimu Nyerere utasaidia wananchi walioko vijijini na mijini kupata nishati ya uhakika na kwa gharama
nafuu na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa ukataji wa miti kwa ajili ya kupata nishati ya kuni na mkaa. Jitihada hizi zitachangia kwa kiasi kikubwa kwenye hifadhi ya mifumo asilia ya kimaumbile/bioanuai.
Awali Waziri Zungu amewatunuku vyeti Wakaguzi wa Mazingira 22 kutoka Wilaya za Mkoa wa Dodoma ambao walishiriki mafunzo yalitolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
pamoja na Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC.
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa tarehe 5 Juni kila mwaka. Kaulimbiu yam waka huu ni ”Tutunze Mazingira: Tukabiliane na Mabadiliko ya Tabianchi”.