Na Masanja Mabula, PEMBA.
WAKULIMA kisiwani Pemba wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwepo na kiwanda cha kutengeneza unga wa sembe kisiwani humo cha KANGAROO SUPER SEMBE kwa kuwekeza katika kilimo cha mahindi ili kukidhi mahitaji ya kiwanda hicho, ambacho kinahitaji zaidi ya tani 50 kwa mwezi.
Ushauri huo kwa wakulima umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Wete Kepteni Khatib Khamis Mwadini wakati wa ziara yake kwenye kiwanda hicho ambapo amewataka wakulima kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha Mahindi kwani mbali na kuzalisha ajira pia soko lake ni la uhakika.
Amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hichi ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Ali abdalla sharif amesema wanalazimika kufuata malighafi nje ya Kisiwa cha Zanzibar kutokana na kutokuwepo wa malighafi hiyo visiwani humo.
Baadhi ya wananchi wamekizungumzia uwepo wa kiwanda hicho wamesema utawapunguzia gharama wafanyabiashara ya kufuata unga wa sembe nje ya Kisiwa hicho na kuwataka wananchi kuhamasika kulima kilimo cha mahindi.
Kiwanda hicho kwa siku kinazalisha tani themanini(80) ambazo hata hivyo hazikidhi mahitaji ya soko la ndani.