Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe (wa pili kushoto) akikabidhi msaada wa kompyuta tano na printa moja zenye thamani ya Sh.milioni 9.7 katika Shule ya Sekondari ya Ilongero iliyopo Wilaya ya Singida mkoani Singida. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri, Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru na Mkuu wa shule hiyo, Ramadhan James.
Vifaa hivyo vikikabidhiwa. Wengine ni viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo.
Hapa wakionesha ishara ya mshikamano.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe ametoa msaada wa kompyuta tano na printa moja zenye thamani ya Sh.milioni 9.7 katika Shule ya Sekondari ya Ilongero iliyopo Wilaya ya Singida mkoani Singida.
Mattembe akizungumza juzi wakati akitoa msaada huo alisema umelenga kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kuhakikisha mpango wa utoaji elimu bure kwa kila mtoto hapa nchini unaendelea kufanikiwa.
” Niliona ni muunge mkono Rais wetu kwa kutoa msaada huu kwa wanafunzi wetu hawa wa Sekondari ya Ilongero kusoma masomo ya ICT kwa njia ya vitendo ili waendane sanjari na ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.” alisema Mattembe.
Mattembe alisema dunia hivi sasa imepiga hatua kubwa ya maendeleo hasa katika matumizi ya teknolojia hivyo wanafunzi wetu wasipojifunza masomo ya ICT watachelewa kuyafikia mafanikio.
” Hivi sasa kila jambo linalofanyika linafanyika kwa njia ya mtandao ambapo ni lazima muhusika ajue kutumia kompyuta au simu sasa tukiacha kuwekeza katika masomo hayo itakuwa changamoto kubwa kwa watoto wetu.” alisema Mattembe.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri ambaye alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano hayo akizungumza wakati akimkabidhi msaada huo mkuu wa shule hiyo, Ramadhan James, alisema msaada huo umekuja wakati muafaka ambao utawasaidia wanafunzi kujifunza masomo kwa ufasaha hasa kipindi hiki ambacho dunia inaunganishwa na mitandao.
“Pamoja na yote katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona kompyuta hizi zitasaidia wanafunzi wetu kujifunza kwa njia ya mtandao bila ya kuwa darasani hivyo napenda kumshukuru Mhe.Mattembe kwa kuona mbali na kutoa msaada huu ambao umefika kwa wakati muafaka” alisema Mulagiri.
Wageni waalikwa wengine katika makabidhiano ya kompyuta hizo walikuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, William Nyalandu, Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru, Diwani Viti Maalumu wa kata hiyo, Mwanamosha Bakari, Diwani Viti Maalumu, Salma Kundya na Katibu Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Singida, Naomi David.
Wengine walioshuhudia makabidhiano hayo ni walimu wa shule hiyo,wenyeviti wa Serikali za mitaa wa Ilongero na baadhi ya wazazi.