Na Silvia Mchuruza, Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti amesema kuwa serikali inaunga mkono wanunuzi binafsi kwenye zao la Kahawa japo wamechelewa sana kuingia sokoni kuanza kununua kahawa za wakulima.
Gaguti ameyasema hayo leo tarehe 4 Juni 2020 wakati akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam ofisini kwake Mkoani mjini Bukoba na kuwataka wanunuzi hao kuingia sokoni.
“Serikali haitaki maneno inataka wakulima wapate fedha kwa wakati, wanunuzi binafsi wamechelewa sana kuingia sokoni tulitegemea waingie sokoni tangu mwezi wa pili waanze kuingia makubaliano na Vyama vya Ushirika, lakini hawajachelewa sana waje ofisini kwangu waeleze wazi wanataka kahawa kiasi gani kisha tuingie makubaliano ya awali” Alikaririwa Rc Gaguti
Ameongeza kuwa Wanunuzi binafsi wanapaswa kujitokeza hadharani watoe ofa yao ikieleza kuwa wanataka kununua kiasi gani cha kahawa ili kuhuisha maneno yao kwa matendo.
Awali katika mkutano uliofanyika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Richard Ruyango alisisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia mipango yake katika zao la Kahawa hususani kuimarisha usimamizi madhubuti ili kuwa na kahawa Bora kwa kuongeza tija na Uzalishaji.
Kuhusu wanunuzi binafsi amesema kuwa wanapaswa kutekeleza sheria, na taratibu za ununuzi wa zao hilo ikiwa ni pamoja na kuwa na kibali cha ununuzi kinachotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halamshauri husika pamoja na kuwa na leseni ya Biashara inayotolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam akizungumza na wanunuzi wa Kahawa katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba ameweka bayana utaratibu wa ununuzi wa kahawa ya wakulima katika Mkoa wa Kagera ambapo Wanunuzi watakaoruhusiwa kununua kahawa ni wale waliopata leseni za kununua kahawa kwa mujibu wa kanuni ya 26 ya Kanuni za Kahawa 2013.
Ameongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri watapaswa kutoa vibali kwa haraka kwa wanunuzi wenye sifa ili kuiwezesha Bodi kutoa leseni kwa wakati.
Kadhalika, Prof Jamal amesisitiza kuwa Wakurugenzi wanapaswa kuwajulisha kwa maandishi waombaji watakaonyimwa vibali wakiweka bayana sababu za kutowapatia vibali na nakala ya barua hiyo iwasilishwe Bodi ya Kahawa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wao wanunuzi wa kahawa wamepongeza uamuzi huo wa serikali kuwaruhusu kununua kahawa kwenye vyama vya Ushirika huku wakiahidi kutekeleza taratibu na sheria za ununuzi wa Kahawa.
Akizungumza kwa niaba ya wanunuzi hao Afisa Masoko wa Kampuni ya Karagwe Estate Ltd Ndg Kamanzi Mombeki amesema kuwa Kampuni hiyo imejipanga kurejea tena katika ununuzi wa kahawa baada ya kusimamia kwa zaidi ya miaka miwili kufanya Biashara hiyo.
“Sisi kama Kampuni tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa kurejesha wanunuzi binafsi kununua kahawa hivyo nasi tumerejea kwa nguvu na Ari kubwa katika ununuzi wa kahawa” Alisema Mombeki
Amesema kuwa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuhusu wanunuzi binafsi wakati akizungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamisheye, Kemondo Muleba, Nyakabango na Kyamyorwa mkoani Kagera tarehe 11 Julai 2019 yalilenga kuongeza ushindani wa kibishara jambo ambalo linamnufaisha zaidi mkulima mwenyewe.
Mombeki ameonyesha kuwashangaa watu wanaopinga maelekezo ya Mhe Dkt Magufuli yenye lengo la kumkomboa mkulima.