Mkuu wa wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga (kushoto) akipokea baiskeli iliyotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu (SIMCU) kwa mtoto Ritha Elias mwenye ulemavu wa miguu(hayupo pichani) kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa SIMCU, Bw. Emmanuel Mwerere makabidhiano hayo yamefanyika sambamba na makabidhiano ya fedha taslimu shilingi 300,000/= Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga (kulia) akimkabidhi mtoto Ritha Elias mwenye ulemavu wa miguu fedha taslimu shilingi 300,000/= iliyotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) kwa ajili ya kumsaidia mtoto huyo katika elimu makabidhiano ambayo yamefanyika sammbamba na makabidhiano ya baiskeli kwa ajili yamtoto huyo Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) Bw. Emmanuel Mwerere akizungumza kabla ya kukabidhi baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= kwa ya kumsaidia mtoto huyo katika elimu, makabidhiano ambayo yamefanyika kati ya Uongozi wa SIMCU na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.
Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) wakiwa katika picha ya pamoja na mtoto Ritha Elias(mbele), viongozi wa Mkoa wa Simiyu, mlezi wa mtoto huyo (kulia) Perpetua Mtaima(kulia) mara baada ya uongozi wa SIMCU kumkabidhi mtoto huyo baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= Juni 04, 2020 kwa ajili ya kumsaidia katika elimu.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahimu Kadudu kabla ya Uongozi wa Chama Kikuu cha ushirika Simiyu(SIMCU) kukabidhi baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= kwa ya kumsaidia mtoto huyo katika elimu, makabidhiano ambayo yamefanyika kati ya Uongozi wa SIMCU na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) na Afisa Elimu watu wazima mkoa wa Simiyu, Mwl. Jusline Gilbert wakiwa katika picha ya pamoja na mtoto Ritha Elias mara baada ya uongozi wa SIMCU kumkabidhi mtoto huyo baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= Juni 04, 2020 kwa ajili ya kumsaidia katika elimu.
*****************************
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu (SIMCU) kimetenga jumla ya shilingi milioni 36.7 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu na afya katika Mkoa wa Simiyu.
Hayo yamesemwa na makamu mwenyekiti wa SIMCU, Bw. Emmanuel Mwerere Juni 04, 2020 Mjini Bariadi wakati akikabidhi fedha na baiskeli kwa mtoto Ritha Elias (08) mwenye ulemavu wa miguu.
“Chama kikuu cha ushirika mkoa wa Simiyu kimetenga jumla ya shilingi 36,700,000/= kati ya hizo shilingi 24,000,000/= itasaidia elimu kwa watoto wenye ulemavu shilingi 12,000,000/= tutanunua mashuka kwa ajili ya Hospitali zote za mkoa wa Simiyu na shilingi 700,000/= kwa ajili ya kumsaidia mtoto Ritha Elias ambaye ni mlemavu wa miguu,”alisema Mwerere.
“SIMCU leo tunamkabidhi mtoto Ritha Elias kiasi cha shilingi 300,000/= ikiwa ni ada ya shule na nauli ya kwenda na kurudi na baiskeli yenye thamani ya shilingi 400,000/= ambayo itamsaidia akiwa nyumbani na shuleni, “aliongeza Mwerere.
Aidha, Mwerere ameongeza kuwa mpango huo ni mwendelezo wa shughuli za chama hicho katika kusaidia jamii huku akiongeza kuwa awali walitoa zaidi ya shilingi milioni 3 kwa ajili ya chakula cha wanafunzi waliokuwa kwenye kambi za kitaaluma.
Katika hatua nyingine Mwerere ameomba makampuni ya pamba yaliyonunua pamba msimu wa wa mwaka 2018/2019 kulipa fedha za ushuru kiasi cha shilingi milioni 729,520,255.
Awali akiongea kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ameipongeza SIMCU kwa kutenga fedha hizo na kurudisha shukrani kwa jamii ikiwemo kumsaidia mtoto mwenye ulemavu wa miguu.
‘’Baadhi ya vyama vya ushirika vinafanya vizuri lakini fedha zao zinaishia kwenye posho na vikao, niwapongeze kwa kutenga kiasi cha milioni 36.7 kwa ajili ya huduma za kijamii ,leo mmekabidhi baiskeli kwa mtoto huyu mwenye ulemavu na mmemwingiza katika mpango wa kumsomesha mpaka mwisho wa masomo yake niwapongeze sana na kingine huyu binti ana kipaji cha kuchora ni mchoraji mzuri sana ’’ alisema Kiswaga.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Simiyu, Ibrahimu Kadudu amesema kurudisha kwa jamii sehemu ya faida ambayo vyama vya ushirika vinapata huo ndio umuhimu wa ushirika, ambapo amebainisha kuwa pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya elimu na afya, awali SIMCU ilichangia fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya janga la CORONA.
Kwa upande wake bibi wa mtoto wa Ritha Elias, Perpetua Mtaima amesema mtoto huyo alizaliwa akiwa hana miguu yote miwili huku akiongeza kuwa pamoja na ulemavu huo mtoto huyo ana uelewa wa vitu vingi japokuwa ni mdogo na kwa hivi sasa anasoma darasa la tatu katika shule ya watoto wenye ulemavu ya Jeshi la Wokovu iliyopo jijini Dar es salaam na amekuwa akifanya vizuri darasani.
“Nilikuwa naomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa wilaya ili mtoto huyu apate elimu na hana miguu nikushukuru sana baba (mkuu wa wilaya ) na mjukuu wangu huyu amekuwa akiniambia siku moja atanibeba kwenye gari lake pia atanipeleka ofisini kwake na akimaliza masomo atapata kazi…nawashukuru wote mlionisaidia kunipatia nauli ya kumpeleka Dar es Salaam’’ alisema Perpetua.