Home Mchanganyiko AFISA CHANJO HANANG’ ATIWA HATIANI KWA UBADHIRIFU

AFISA CHANJO HANANG’ ATIWA HATIANI KWA UBADHIRIFU

0

********************************

MTUMISHI wa Serikali ambaye ni mratibu wa chanjo wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, Mkojera Philemon amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi 50,000 kwa kila kosa kwenye makosa saba ya ubadhirifu wa fedha za chanjo. 
Hukumu hiyo ilitolewa Mei 29 na hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Hanang’ Aman Shao baada ya mshtakiwa huyo Philemon kuonekana kuwa ana hatia. 
Kwenye mashtaka hayo sana Philemon alitiwa hatiani kwa ubadhirifu wa kujipatia fedha shilingi 4,425,000 kwa kuorodhesha majina ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwa aliwalipa posho jambo ambalo siyo kweli. 
Waendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Isdory Kyando na Evelyine Onditi walidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo mwaka 2014 na kufikishwa mahakamani mwaka 2018 katika kesi hiyo namba 89/2018.
Waendesha mashataka hao walidai kuwa katika mashtaka hayo saba, mshtakiwa huyo aliorodhesha majina ya watumishi wa Halmashauri hiyo kuwa aliwalipa fedha kwa ajili ya safari ya chanjo ya surua na rubela huku akijua siyo kweli. 
Baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili hakimu Shao aliridhika kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo hivyo kumpa adhabu ya kwenda jela miezi 12 kwa kila kosa. 
Hata hivyo, hakimu Shao alisema katika hukumu hiyo mshtakiwa huyo anaweza kulipa faini ya shilingi 50,000 kwa kila kosa kati ya makosa hayo saba ili kuepuka kifungo cha mwaka mmoja. 
Philemon alilipa faini ya shilingi 350,000 kwa kila kosa shilingi 50,000 kati ya makosa yote saba hivyo kukwepa kutumikia kifungo. 
Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari alisema Philemon alipata adhabu hiyo inayoonekana kuwa ina unafuu kwa kuwa makosa aliyoyatenda mwaka 2014 kabla sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 1/2007 haijafanyiwa marekebisho.  
Makungu aliwataka watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kufahamu kuwa kwa nia thabiti ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa nchini, Bunge lilipitisha sheria namba 3/2016 na kutiwa saini na Rais John Magufuli Julai 7 mwaka 2016.
Alisema sheria hiyo ilianza kutumika rasmi Julai 8 mwaka 2016 baada ya kutangazwa katika gazeti la Serikali. 
Alisema katika sheria hiyo makosa karibu yote ya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 yakiwemo ya ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka, uchepuzi na matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri kama alivyofanya Philemon yamekuwa makosa ya uhujumu uchumi. 
“Kwa msingi huo ukishapatikana na hatia mahakamani kwa makosa ya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 yaliyotendeka kuanzia Julai 8 mwaka 2016 adhabu iliyopitishwa na Bunge ni kifungo kisichopungua miaka 20 jela au kisichozidi miaka 30 jela,” alisema Makungu. 
Alisema pamoja na adhabu hiyo sheria namba 3/2016 inaelekeza pia mali zilizopatikana kutokana na makosa ya rushwa zitataifishwa na kurejeshwa Serikalini. 
“Katika mabadiliko hayo ya sheria hakuna mbadala wa faini, hivyo ni rai yangu kwa watumishi wa umma kujiepusha na vitendo vya rushwa na wale wenye masikio lakini hawataki kusikia wataanza kukumbana na adhabu hiyo kali hivi karibuni,” alisema Makungu.