Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee(Kushoto) akikabidhi funguo za malori mapya kwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, SACP. Chacha Bina leo Juni 1, 2020 katika Viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, jijini Dodoma.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee akijaribu kuliwasha moja ya lori kabla ya kukabidhi malori mapya matatu kwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, SACP. Chacha Bina(hayupo pichani) leo Juni 1, 2020 katika Viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, jijini Dodoma.
Muonekano wa malori mapya matatu yaliyokabidhiwa kwa ajili ya shughuli za Kikosi ujenzi cha Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, leo Juni 1, 2020 katika Viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, jijini Dodoma.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee(wa pili toka kulia) akifanya mahojiano mafupi na wanahabari mara baada ya makabidhiano ya malori ya Shirika la Uzalishaji mali la Magereza leo Juni 1, 2020 katika Viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, jijini Dodoma(Picha zote na Jeshi la Magereza).
…………………………………………………………………………
Na ASP. Lucas Mboje, Dodoma.
KATIKA kuimarisha shughuli za Kikosi ujenzi cha Shirika la uzalishaji mali la Magereza(SHIMA). Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee amekabidhi malori matatu (03) mapya aina ya TATA yenye thamani ya zaidi ya milioni 400 Tsh ambayo yatakayotumika katika miradi mbalimbali ya ujenzi ya Shirika hilo hapa nchini.
Akizungumza katika makabidhiano ya magari hayo leo Juni 1, 2020 jijini Dodoma, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Suleiman Mzee amesema kuwa kwa muda mrefu Shirika hilo limekuwa na uhaba wa vitendea kazi ikiwemo magari hali ambayo ilililazimu Shirika kukodi baadhi ya vifaa na mitambo ya ujenzi hivyo kuongeza gharama za uendeshaji pamoja na kulikosesha Shirika mapato katika miradi yake.
“Shirika letu la Uzalishaji Mali la Magereza linasimamia miradi mbalimbali ikiwemo shughuli za ujenzi, kilimo na viwanda vidogovidogo hivyo nimeona ni vyema kuliwezesha Shirika hili malori haya makubwa matutu ili waachane na utaratibu wa kukodi na hivyo naamini wataweza kutengeneza faida katika miradi ya Shirika “, amesema Kamishna Jenerali Mzee.
Aidha, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Suleiman Mzee ameongeza kuwa atahakikisha kuwa katika miradi mbalimbali ya Shirika hilo pamoja na maeneo mengine yenye fursa za kiuzalishaji yanawezeshwa vifaa na nyenzo mbalimbali za kisasa yakiwemo matrekta na mitambo ya uvunaji ili kuongeza na hivyo kutimiza adhima ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu Jeshi la Magereza kujitegemea na kuongeza uzalishaji.
“Shirika la Magereza lina zaidi ya miradi 20 ikiwemo ya kilimo, mifugo, viwanda vidogovidogo na kikosi ujenzi hivyo tutaanza na miradi hiyo ya uzalishaji mali kwa kuwezesha vifaa na mitambo ya kisasasa ili kuongeza tija katika uzalishaji wa miradi hiyo”, amesisitiza Kamishna Jenerali Suleiman Mzee.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, SACP. Chacha Bina akizungumza kwa niaba ya watendaji wa Shirika hilo amemshukru Kamishna Jenerali wa Magereza Suleiman Mzee kwa kuliwezesha Shirika hilo malori matatu ambayo hakika yataimarisha kikosi cha ujenzi cha Shirika hilo katika shughuli zake.
“Nichukue nafasi ya kipekee kumshukru Kamishna Jenerali Suleiman Mzee kwa juhudi zake kubwa ambapo ni katika kipindi kifupi tangu akabidhiwe Shirika letu amewezesha kutukabidhi magari haya kwani awali Kikosi chetu cha ujenzi kilikuwa kina kodi vifaa vya ujenzi hali ambayo ilipelekea Shirika kuwa na gharama kubwa za uendeshaji pamoja na kukosa mapato katika miradi yake, naamini sasa tutaongeza mapato ya Shirika sambamba na kutoa gawaio kwa Serikali”, amesema SACP. Chacha Bina.
Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza lilianzishwa mwaka 1983 kwa Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1974(The Corporation Sole Act No.23/1974) chini ya kifungu cha 3(1) na kanuni zake za mwaka 1983. Malengo ya Shirika hilo ni kuwa Chombo cha urekebishaji wa wafungwa kwa kuwafundisha stadi za kazi na kuwaongezea ujuzi kwa wale ambao tayari wana ujuzi. Pia, Shirika hilo linaendesha shughuli zake kiuchumi na kibiashara kwa kujitegemea(Revolving fund) na lengo jingine shirika hilo ni kuipunguzia serikali mzigo wa gharama za uendeshaji wa magereza.