Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo akikagua ujenzi wa hospitali ya Kilolo katika ziara ya kikazi wilayani humo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo akizungumza na watendaji wa Wilaya ya Kilolo katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Kilolo.
Muonekano wa Mradi wa Maendeleo wa Ujenzi wa Hospitali ya Kilolo.
………………………………………………………………………….
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo, amekagua ujenzi wa Hospitali za Wilaya ya Kilolo na Mufindi ambapo Mkoani Iringa ameonyesha kuridhishwa kwake na ujenzi huo.
Ukaguzi huo ameufanya leo alipokuwa katika ziara ya kikazi wilayani humo akikagua miradi ya maendeleo iliyo chini ya Ofisi ya Rais, Tamisemi.
Jafo ametembelea Hospitali ya Kilolo, Kituo cha Afya Ng’uluhe, na Hospitali ya Wilaya ya Mufindi ambazo ujenzi wake ni matokeo ya mkakati wa serikali wa kuimarisha huduma ya Afya nchini kwa kuzifikia halmashauri ambazo hapo awali hazikuwa na hospitali.
Amesema kwa sasa hospitali mpya 98 zinajengwa maeneo mbalimbali hapa nchini.
Ameagiza ndani ya wiki moja hadi ifikapo tarehe 8 Juni, 2020 hospitali zote 67 za awamu ya kwanza kati ya hospitali 98 zinazojengwa ziwe zimeanza kutoa huduma kwa kuanza na huduma ya wagonjwa nje na huduma ya mama na mtoto (RCH).
“Haiwezekani wananchi waendelee kutaabika kwa kusafiri umbali mrefu kupata huduma wakati tayari miundombinu ya kuanzia kutolea huduma imekamilika,”amsema.
Jafo amesisitiza kwamba kwa hospitali mpya 67 tayari wiki iliyopita serikali imeshapeleka madaktari angalau watatu kwa kila hospitali ili huduma zianze kutolewa.
Katika ziara hiyo, Wananchi wameishukuru sana serikali kwa kuwajengea hospitali hizo nzuri za kisasa na kumuagiza Waziri huyo awafikishie salamu zao za shukran kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilolo(CCM), Venance Mwamoto ameishukuru sana serikali kwa kusikia kilio chake na kufanikisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya, kituo cha Afya Kidabaga na Ruaha Mbuyuni, pamoja na miundombinu ya barabara.