***********************************
Kutokana na mwenendo mzuri na kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu COVID 19 unaosababishwa na virus vya Korona nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alitoa taarifa kwa Umma kwa kuelekeza shughuli zote za Michezo (ikiwemo Michezo ya Kuigiza) zitafunguliwa rasmi kuanzia tarehe 1 Juni, 2020.
Tarehe 27 Mei, 2020 Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Tanzania Profesa Frowin Nyoni, alikutana kwa nyakati tofauti na Menejimenti na Wadau mbalimbali wa Filamu nchini wakiwemo, viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Wazalishaji, Wasambazaji, Wamiliki wa majumba ya sinema, Wasanii na mawakala wa Wazalishaji wa Filamu kutoka nje ya nchi (Fixers) kujadili athari mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Filamu kutokana na uwepo wa ugonjwa wa COVID 19 na kupokea mapendekezo yao, ya namna sahihi ya ushiriki katika Sekta hiyo pindi itakapo anza rasmi.
Katika hatua nyingine, tarehe 28 Mei, 2020 Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Filamu Tanzania, alikutana na Wajumbe wa Bodi hiyo katika kikao cha dharura kujadili mapendekezo mbalimbali yaliyowasilishwa na Menejimenti ya Bodi ya Filamu na Wadau wa Filamu katika kupelekea kurudisha shughuli za Filamu na Michezo ya kuigiza ambapo, mapendekezo kadhaa yalijadiliwa na kuchukuliwa kwa hatua zaidi.
Aidha, Profesa Nyoni aliwapongeza Wadau wa Filamu nchini kwa jitihada chanya wanazozionesha katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID 19 ikiwemo kutumia nafasi zao katika jamii kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo, ambapo aliwataka kuendelea kufanya hivyo hata baada ya Mh. Rais kuruhusu shughuli za Michezo kuendelea.