Home Siasa UWT WILAYA YA UBUNGO YAANZA KAMPENI YA UGAWAJI WA VIFA KWAAJILI YA...

UWT WILAYA YA UBUNGO YAANZA KAMPENI YA UGAWAJI WA VIFA KWAAJILI YA KUJIKINGA NA COVID-19

0

*********************************

JUMUIYA ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Wilaya ya Ubungo imeanza kampeni ya ugawaji wa vifaa kinga kwa wanawake wajasiriamali ili kujikinga na Ugonjwa wa Covid 19 wilayani humo.

Imesema hatua inafuatia kauli ya serikali ya kuwataka wananchi kuendelea kujikinga na ugonjwa huo licha ya kwamba umepungua ili kuutokomeza kabisa.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa vifaa kinga hivyo kwa wanawake wajasiriamali wa Soko la Kuku na Mbogamboga Manzese jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa UWT Ubungo Pili Mustapha, alisema kampeni hiyo imeanza kwa ugawaji wa Barakoa, Vitakasa mikono na ndooo kwa ajili ya kuwekea maji ya kunawa mikono.

“Huu ni uzinduzi tunatarajia kuendelea kugawa kwa wajasiriamali wote wilaya ya Ubungo na kuhakikisha tunafika masoko na maeneo yote, hivyo muendelezo wa kampeni hii utafanywa na ngazi za chini kwa maana majimbo, kata, mitaa na mashina,” alisema.

Alisema awali wameanza na kugawa vifaa hivyo katika soko la Manzese na Mbezi Luis jijini humo na kwamba maeneo mengine yatagawiwa na uongozi wa jumuiya hiyo wa eneo husika.

Kwa upande wake katibu wa UWT wilaya hiyo Janeth Mnyaga, alisema kampeni hiyo inalenga kuunga mkono kauli ya serikali ya kwamba licha ya kupungua kwa Covid 19 nchini lakini ipo haja ya wananchi kuendelea kujikinga ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.

“Sisi tunafanya kuwakumbusha wananchi wasisahau kujikinga, Corona imepungua nchini lakini bado ipo hivyo ni wajibu kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ambazo miongoni mwazo ni pamoja na uvaaji wa barakoa na kutumia vitakasa mikono,” alisema.

Aliipongeza serikali kwa kuruhusu kuendela kwa shughuli mbalimbali za wananchi ili kuwaepushia adha ya ukata kwani walio wengi nchini maisha yao hutegemea sekta zisizo rasmi.

Janeth aliongeza kwa kuwataka wananchi kuacha kuyapuuza masharti na ushauri unaotolewa na serikali pamoja na wataalamu wa afya ili kuendelea kuutokomeza zaidi ugonjwa huo.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya UWT Ubungo Sophia Fitina, aliwataka wananchi wilayani humo kufanya shughuli zao huku wakikumbuka kujikinga na virusi hivyo.

Alisema vita ya kuishinda Corona inahitaji umakini na mapambano mpaka wakati wa mwisho hivyo ahueni iliyopo isiwape watu imani kuwa hakuna haja ya kujikinga.

Aliongeza kuwa wakati tuliofikia ni wa kuishinda vita hiyo, kuacha kujikinga ni kuandaa mazingira ya kushindwa hivyo wananchi wakumbuke kujikinga ndio maana UWT Wilaya hiyo imeona haja ya kuwakumbusha kwa kuwapelekea vifaa kinga hivyo.