NA DENIS MLOWE, IRINGA
MGAHAWA wa kisasa wa The Koffee Shop ulioko manispaa ya Iringa umetoa msaada wa vitakasa mikono 150 na barakao 100 na ndoo 15 kwa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari vya mkoa wa Iringa ili waweze kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Akizungumzia msaada huo mwakilishi wa The Koffe Shop Charles Cosmas kwa niaba ya Mkurugenzi wa mgahawa huo, Ahmed Salim Abri alisema wameamua kusaidia kundi hilo kutokana na mchango wake kwa jamii katika kipindi hiki hiki cha janga la corona.
Alisema kazi za waandishi wa habari zinawahitaji kukutana na watu mbalimbali hivyo wanapaswa kuwa na vifaa vya kujikinga na maambukizi hivyo kwa kutambua hilo mgahawa huo umeamua kutoa kuweza kuwasaidia wanahabari ambao wamesaulika katika jamii licha ya elimu kubwa wanayotoa kwa jamii dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo.
“Katika mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona wanahabari watu muhimu katika kuhabarisha jamii kuhusu maambukizi ya corona hivyo ni imani yetu kuwa barakoa hizi 100, vitakasa mikono na ndoo 15 zitasaidia kwa muda kwenu kuweza kujilinda na kuendelea kuhabarisha mkiwa salama zaidi” alisema.
Alisema kuwa lengo mgahawa ambao uko chini ya makampuni ya Asas ni kusaidia kwa kurudisha kidogo wanachopata kwenye jamii ambayo kwa namna moja au nyingine inatumia malighafi za kampuni hiyo katika matumizi ya kila siku hivyo wanahabari ni wamojawapo ambao ni wateja wakubwa.
Akizungumzia msaada huo Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) Frank Leonard ameipongeza kampuni hiyo kwa kuwakumbuka waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa ambao walikuwa wanapitia changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo katika sehemu zao za kazi na watahakikisha wanatumia ipasvyo huku elimu ikiendelea kutolewa kupitia kuandika.
“Tunaishukuru Mgahawa wa The Koffee Shop kwa kwa msaada huu wa Barakoa 100 ndoo na vitakasa mikono kwani zitatusaidia sana katika kipindi hiki kigumu naamini sasa tutafanya kazi kwa uhuru na hata tukiandika habari na makala za kusisitiza uvaaji barakoa na matumizi ya kunawa mikono tunaonekana kwa mfano,” alisema
Leonard alisema kuwa mbali na kupewa msaada huo mkurugenzi wake Ahmed Abri amekuwa ikiwaunga mkono mara kwa mara na ni msaada mkubwa kwenye jamii ya mkoa wa Iringa na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kushirikiana katika kusaidia makundi mbalimbali.