Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst) Mathew Mwaimu (kulia) akimkabidhi Kamishna wa
Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela (Kushoto) barua ili
kuimarisha ushirikiano baina ya THBUB na Sekretarieti ya Maadili.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst) Mathew Mwaimu (kulia) akiongea na Kamishna wa
Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela (Kushoto)
alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma jana. Lengo la ziara hiyo ya THBUB ni
kuimarisha ushirikiano na Sekretarieti ya Maadili.
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela
(Kushoto) akiteta jambo na Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya
(Kulia) muda mfupi mara baada ya kumaliza kikao.
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela
(Kulia) akimsindikiza Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst) Mathew Mwaimu (kushoto) mara
baada ya kumaliza mazungumzo yao.
****************************
Na Mbaraka Kambona,
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela
amezishauri taasisi zinazosimamia utawala bora kushirikiana kwa karibu ili waweze
kutekeleza majukumu yao vizuri.
Jaji Nsekela alitoa rai hiyo katika ofisi yake jijini Dodoma jana alipokutana na Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji (Mst) Mathew Mwaimu.
Alisema kuwa taasisi hizo zimekuwa na mazoea ya kushirikiana kwa ukaribu wakati wa
sherehe za maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu, jambo ambalo alisema
kuwa haipaswi kuwa hivyo na badala yake taasisi hizo ziimarishe ushirikiano huo wakati
wote.
Aliongeza kuwa kufanya kazi kwa ukaribu na kubadilishana taarifa wakati wa kutekeleza
majukumu yao kutasaidia taasisi hizo kuainisha mipaka yao ya kiutendaji ambapo
itawawezesha kujiepusha na muingiliano wa shughuli zao.
“Kuna umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu kati yetu, hii itatusaidia kubadilishana
taarifa ambazo zitatusaidia kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo”, Jaji Nsekela alieleza.
Aliendelea kusema kuwa kimsingi majukumu ya taasisi hizo yanafanana, kwani zote ni
taasisi za uchunguzi, tofauti iliyopo ni kwamba THBUB inashughulikia masuala ya haki za
binadamu, Sekretarieti ya Maadili inasimamia maadili ya utumishi wa umma, TAKUKURU
wao wanachunguza masuala ya rushwa na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali
inasimamia matumizi ya fedha za umma.
Aliongeza kuwa kuna haja ya taasisi hizi kubadilishana uzoefu wa mara kwa mara ili kila
mmoja aelewe mipaka ya mwenzake jambo ambalo litawasaidia kuepuka muingiliano wa
majukumu yao.
Aidha, Jaji Nsekela aliishauri THBUB kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake kwa
kuzingatia maadili kwa sababu hiyo ndio njia pekee itakayowawezesha kutoa huduma kwa
wananchi bila malalamiko.
“Katiba imewapa mamlaka ya kulinda na kuhamasisha haki za binadamu na misingi ya
utawala bora nchini, tumieni mamlaka hayo kwa kutoa huduma bora kwa Wananchi huku
mkizingatia maadili”, Jaji Nsekela alisisitiza
Akiongea mapema, Jaji Mwaimu alieleza kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha ushirikiano
na Sekretarieti ya Maadili, lakini pia kuwakumbusha wananchi kuwa THBUB ipo kwa ajili
ya kuwasaidia.
Jaji Mwaimu aliendelea kueleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita THBUB
imekuwa ikitekeleza majukumu yake bila ya uongozi kwa maana ya Makamishna jambo
ambalo liliathiri utendaji wa taasisi hiyo.
“THBUB ni huru, hatupaswi kuchukua upande tunaposhughulikia masuala ya uvunjifu wa
haki za binadamu na misingi ya utawala bora, jukumu letu la msingi ni kusaidia wananchi
kupata haki zao”, Jaji Mwaimu ilifafanua