Home Mchanganyiko NHIF sasa imetukomboa- Wamachinga 

NHIF sasa imetukomboa- Wamachinga 

0

Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda akizindua mpango wa Machinga Afya unaotoa fursa kwa machinga kujiunga na huduma za matibabu kwa gharama nafuu.

Sehemu ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF.

Mwanachama kupitia mpango wa Machinga Afya akifuarahia baada ya kupokea kadi yake ya matibabu.

Mama Anne Makinda akikabidhi kadi kwa wanachama wapya kupitia mpango wa Machinga Afya.

Mwenyekiti wa Bodi Mama Anne Makinda akishuhudia uwekaji wa Saini wa Mkataba wa Makubaliano ya huduma hiyo kati ya Machinga na NHIF

Zoezi la utiaji wa saini likiendelea.

……………………………………………………..

Na Mwandishi Wetu

WAMACHINGA nchini wamesema kuwa, kitendo cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kukamilisha na kuzindua rasmi mpango wa huduma za matibabu kwa kundi hilo unaojulikana kama Machinga Afya ni kuwakomboa kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania Bw. Stephen Lusinde, Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa mpango huo ulioambatana na kusaini mkataba wa makubaliano kati ya Mfuko na Chama cha Wamachinga wa namna ya uendeshaji wa huduma kwa kundi hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, amesema kwamba kitendo cha kuzinduliwa kwa mpango huo ni sawa na Machinga kuzaliwa upya wakiwa na matumaini ya ulinzi wa afya zao na uchumi wao.

“Hakika siku ya leo kwetu ni sawa na kuzaliwa upya, hapo awali hatukuwa na uhakika wowote wa ulinzi wa afya zetu, kupewa fursa hii na Mfuko inatuhakikishia usalama zaidi wa mitaji yetu lakini uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote,” alisem Bw. Lusinde.

Alitumia fursa hiyo kutoa pongezi zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo amehakikisha chini ya uongozi wake kunakuwa na uhakika wa huduma zote za kijamii ikiwemo suala la afya ambalo ni suala nyeti.

“Miaka ya nyuma sisi tulijiona kama ni kundi ambalo limetengwa lakini kwa kitendo hiki cha sisi kuanza kutumia huduma za NHIF sasa tunatembea kifua mbele na katika hili naomba niwapongeze sana Mfuko kwa kuhakikisha hili linafanikiwa na Wamachinga wote nchini wamepokea hili kwa furaha kubwa,” alisema Bw. Lusinde.

Akizindua mpango huo, Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda alisema kuwa tendo la uzinduzi huo ni matokeo chanya ya kazi kubwa iliyofanywa kuhakisha kila kundi la wananchi linakuwa na fursa ya kujiunga na huduma za matibabu.

Alisema kuwa kauli ya HAPA KAZI TU iliyotolewa mwaka 2015 na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli imekuwa na matokeo makubwa sana ambayo kila mmoja kwa sasa anaweza kuyaona kwa macho.

Alisema kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya uboreshaji wa hospitali nchini na huduma za matibabu kwa ujumla hatua inayowezesha upatikanaji wa huduma zote za matibabu kirahisi na kuondoa changamoto zilizokuwepo awali zikiwemo za ukosefu wa dawa.

“Mfuko umejipanga sana kuwahudumia wananchi na kuwafikia katika maeneo yao, hivyo natoa wito kwa watoa huduma kuhakikisha wanawahudumia wanachama kulingana na maadili yao ya kazi,” alisema Mama Makinda.

Aidha aliwaomba wananchi kuwa na kipaumbele katika kuwekeza kwenye afya zao badala ya kuelekeza fedha katika mambo mengine kama ya kuchangia harusi na sherehe zingine.

Akielezea namna Mfuko ulivyojipanga kutoa huduma kwa kundi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga amesema mkakati uliopo ni kutoa huduma bora kwa wanachama na kuendelea kuwafikia wananchi ili waweze kujiunga.

“Leo tunaanza na kundi la Wamachinga wa Kariakoo ambao wana utaratibu mzuri sana wa kuratibu wanachama wao na mpango huu umelenga kuwawezesha wajasiliamali hawa kwa gharama ya shilingi 100,000 tu kwa mwaka hivyo niwahakikishie kuwa upatikanaji wa huduma ni wa uhakika kabisa,” alisema Bw. Konga.