Shirika la AGAPE ACP la mkoani Shinyanga linalotetea Haki za Watoto na Wanawake limetoa elimu ya ukatili wa kijinsia pamoja na namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, kwa waelimishaji rika Kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la Agape John Myola, amewataka waelimishaji rika hao kwenda kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia na Corona kwa wananchi kwa ufasaha ili kuokoa maisha yao.
Amesema katika kipindi hiki cha janga la Corona, wananchi wanapaswa kuendelea kupewa elimu ya kujikinga na maambukizi ya COVID -19 hayo pamoja na ukatili wa kijinsia, ili jamii ibaki kuwa salama.
“Tumaini letu sisi Shirika la AGAPE ACP ni kuona nyie waelimishaji rika mnatoa elimu ya ukatili wa kijinsia, na Corona kwa wananchi, ambayo mmepewa na wataalamu wa afya ili kuokoa maisha yao,” amesema Myola.
“Msipotoa elimu hii vizuri kwa wananchi, dhambi itawatafuna ninyi kwa sababu ujuzi mmepewa na hamjakwenda kuelimisha wengine ili kuwaweka kuwa salama, katika kipindi hiki kigumu cha janga la Corona, hivyo naomba mtoe elimu hii vizuri kwa wananchi”, ameongeza.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mwamala Sophia Philbert, amewataka wananchi pale wanapohisi kuna mtu ana dalili za maambukizi ya virusi vya Corona, watoe taarifa kwa wataalamu na siyo kwenda kutibiwa kwa waganga wa kienyeji.
Kwa upande wake Mhudumu wa afya kutoka kituo cha afya Samuye Ilambona Alfred, amewataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona, kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, na kuepuka mikusanyiko.
Aidha Afisa Mradi wa Kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa Shirika hilo la AGAPE ACP Sofia Rwazo , amewataka waelimishaji rika kuendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili ndani ya jamii ili kumaliza matukio hayo.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ACP John Myola akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa elimishaji rika Kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Alhamis Mei 28,2020. Picha zote na Marco Maduhu – Malunde 1 blog
Mhudumu wa afya kituo cha afya Samuye Ilambona Alfred akitoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.
Afisa Mradi wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto, Sofia Rwazo kutoka Shirika hilo la Agape, akiwataka waelimishaji rika, kuendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili ndani ya jamii ili kumaliza matukio hayo.
Wa kwanza kushoto Mratibu wa miradi kutoka Shirika la Agape Peter Amani na Waelimishaji rika wakiwa kwenye kikao hicho.
Afisa tarafa ya Samuye Ntarle Magese akisisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona pamoja na kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mwamala Sophia Philibert akizungumza kwenye kikao hicho.
Wajumbe wakipiga picha ya pamoja na watendaji wa Shirika la AGAPE ACP pamoja na mkurugenzi wa shirika hilo John Myola, (katikati mwenye nguo nyeusi).
Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 blog