Home Mchanganyiko WIMBI LA TEMBO LAVAMIA BAADHI YA MAENEO YA KIWANGWA, KANDO YA MTO...

WIMBI LA TEMBO LAVAMIA BAADHI YA MAENEO YA KIWANGWA, KANDO YA MTO WAMI-MALOTA

0

********************************

NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE
WIMBI la wanyama aina ya tembo ,limevamia baadhi ya maeneo yaliyopo kando ya mto Wami ,kata ya Kiwangwa ,Chalinze wilaya ya Bagamoyo,mkoani Pwani hali inayosababisha uharibifu wa mazao na hasara kubwa kwa wakulima wa maeneo hayo.

Hii ni mara ya tano kutokea kwa wimbi la wanyama tembo ambapo kila mwaka wamekuwa wakijitokeza wakitokea mbuga ya wanyama ya Saadan na kupitia kando ya mto Wami na kuingia kwenye maeneo ya wananchi.

Diwani wa kata ya Kiwangwa Malota Kwaga ,alisema hayo wakati wa kikao cha baraza la madiwani Chalinze kwenye kikao cha taarifa ya kata kwa kata na kueleza tembo wanaleta kero kwa wananchi hasa wakulima ambao tegemo lao kubwa ni kilimo. 

Alieleza, wanyama hao wamekuwa wanaharibu mazao ya mananasi kwenye maeneo ya watu, migomba,mahindi na mpunga lakini hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza .

Malota ,alieleza kwamba ,wameshatoa taarifa kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze ili watalaamu kitengo cha wanyama pori na maliasili wafike kuondoa tembo hao lakini bado hawajafika ambapo tembo hao wameshavamia kipindi cha wiki moja sasa.

“Miezi sita iliyopita hakukuwa na kadhia hii ,ila ni changamoto ya kila mwaka ,hii ni mara ya tano hivi ,ni vyema watumishi hao wakapiga kambi eneo la tukio ili kuondoa usumbufu kwa jamii”;

Malota aliomba serikali isaidie changamoto hiyo kwakuwa imekuwa kero kwa wakulima waliopo kando ya mto Wami ikiwemo kitongoji cha Minazi na Misani.

Ipo changamoto nyingine ya baadhi ya barabara kutopitika kutokana na mvua zilizonyesha ,lakini baadhi tumeshazifungua licha ya barabara nyingine kuingizwa katika bajeti ya TARURA ikiwa ni pamoja na barabara ya Kiwangwa -Wami na Bago kwenda Talawanda na kujenga kituo cha polisi Msinune.

Diwani huyo wa Kiwangwa alifafanua, ipo changamoto nyingine ya ukosefu wa kituo cha afya ambapo wanategemea serikali itatatua changamoto hiyo kutokana na serikali ya awamu ya tano kuwa sikivu .

Licha ya changamoto hizo ,lakini alipoingia madaraka alikuta tatizo kubwa la upungufu wa madarasa katika elimu msingi na sekondari ambapo madarasa yamejengwa na kupunguza tatizo la maabara kwenye shule za sekondari.