Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imemwita Dk. Imni Patterson, Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Marekani hapa nchini kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo Ubalozi huo umekuwa ukiyaandika katika mitandao yake ya kijamii bila ya uthibitisho.
Kaimu Balozi huyo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwenye Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Katibu Mkuu ameeleza masikitiko yake kutokana na namna ambavyo Ubalozi huo umekuwa ukitoa taarifa mbalimbali za ushauri wa kiusafiri (travel advisory) zinazoandikwa na kusambazwa na Ubalozi wa Marekani kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo suala la namna Tanzania inavyoshughulikia ugonjwa wa COVID-19.
Akitolea mfano Katibu Mkuu amezitaja taarifa zilizotolewa na Ubalozi huo siku ya Jumatano 13 Mei, 2020 na ya siku ya Jumatatu 25 Mei, 2020 kwenye mtandao wa “Twitter” wa Ubalozi huo ambazo zote zilionekana kukusudiwa kutoa tahadhari kwa raia wa Marekani waliopo nchini na wanaotarajia kuja Tanzania kuwa jiji la Dar es Salaam siyo salama kutokana na kuwepo idadi kubwa ya wagojwa wa COVID-19.
Tahadhari hizo pia zimeendelea kudai kuwa hospitali nyingi jijini Dar es Salaam (bila ya kuzitaja hospitali hizo) zimefurika wagonjwa wa COVID-19 jambo ambalo siyo kweli na linauwezekano wa kusababisha taharuki kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi ilhali hali halisi sivyo ndivyo inavyodaiwa.
Katibu Mkuu amemjulisha Kaimu Balozi kuhusu umuhimu wa Ubalozi kutoa taarifa zilizothibitishwa hususan kwa sababu serikali haina kizuizi cha aina yoyote kwa Mabalozi kutafuta na kupata taarifa sahihi na zenye ukweli.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amemshukuru Kaimu Balozi huyo kwa ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Marekani katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama na maeneo mengine ya maendeleo.