Ofisa Miradi wa Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD), Richard Magodi (kushoto) akikagua uwepo wa chanjo kwenye jokofu la kutunzia chanjo Zahanati ya Kicheba A. Kulia ni Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Tanga, Seif Shaibu.
Ofisa Miradi wa Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD), Richard Magodi (kushoto) akikagua uwepo wa chanjo kwenye jokofu la kutunzia chanjo Zahanati ya Kicheba A. Kulia ni Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Tanga, Seif Shaibu.
Bi. Rukia Sewaja mkazi wa Kicheba akisafisha mikono yake tayari kwa huduma ya chanjo kwa mwanae kwenye Zahanati ya Kicheba A.
………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum – Muheza
WANANCHI na watoa huduma za Chanjo katika Halmashauri ya Muheza Mkoani Tanga, wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wake wakiwemo Engender Health kupitia Meck Sharp & Dohme B.V (MSD) kwa upelekaji elimu na uhamasishaji huduma za ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara ya kukagua huduma za chanjo ya HPV inayokinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa saratani ya kizazi kwa Wasichana wenye umri wa miaka 14 pamoja na chanjo nyingine
Ziara hiyo iliyoongozwa na Ofisa Miradi kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD), Richard Magodi na maofisa wa Chanjo Mkoa huo, walitembelea maeneo ya pembezoni (Vijijini ) ambapo huduma zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Vituo hivyo vya Chanjo ni pamoja na Zahanati ya Kicheba A, Zahanati ya Nkumba kijiji cha Kilometa 7 na Kituo cha Afya Ubwari ambapo baadhi ya Wananchi walijitokeza kupatiwa huduma za chanjo huku wakichukua tahadhari kubwa.
“Sisi wazazi ndio tulio na jukumu kubwa la kulinda watoto wetu. Tunaishukuru Serikali na watu wote ikiwemo nyie wageni wetu mliokuja kututembelea na kujua kama tunapata chanjo ama la!.
“Tunapata elimu za kujikinga na magonjwa na pia watoto wetu wanapatiwa chanjo wakati huu ambao pia kuna Corona”. Alisema Bi. Rukia Sewaja mkazi wa Manzese Kicheba.
Kwa upande wake Muuguzi mkunga wa Zahanati hiyo ya Kicheba A, Spora Kabati alipongeza ugeni huo wa mpango wa Taifa wa Chanjo na wadau wake Engender Health kufika na kujionea utoaji wa huduma na kutoa uhamasishaji.
“Tumechukua tahadhari ya kujilinda na kuwalinda wengine. Watu wanaoleta watoto wao lazima kwanza wasafishe mikono na pia wavae barakoa na kuzingatia umbali mtu na mtu” Alisema Bi. Spora Kabati.
Nao baadhi ya akina mama wa Kijiji cha Kilometa 7, waliofika kituo cha Chanjo Zahanati ya Nkumba, walipongeza namna wanavyopatiwa huduma.kwa uangalifu na kuondolewa hofu.
“Awali tuliogopa kuleta watoto wetu kwenye chanjo.
Lakini tunashukuru Serikali tumekuta mazingira mazuri na tumepewa na elimu ya kujikinga na kukinga wengine na Corona” Alisema Bi. Asha Suleiman.
Mzazi mwingine aliyemfikisha mwanae kupatiwa chanjo kituoni hapo aliomba Serikali kuendelea kutoa elimu vijijini kwani huko kuna wananchi wengi.
Naye Muuguzi Mkunga anashughulikia huduma za Chanjo wa Zahanati hiyo Bi. Magdalena Chombo alisema wamekuwa wakishirikiana na wadau kijijini hapo kutoa elimu sahihi ya Corona pindi wakinamama hao wanalofika kupatiwa huduma za chanjo.
Kwa upande wake Ofisa Miradi Mpango wa Taifa wa Chanjo, Richard Magodi aliwataka watoa huduma hao kuzingatia muongozo wa kujilinda na kuwalinda wengine na Corona sambamba na uingizaji wa taarifa katika mfumo wa kielektroniki unaotumiwa katoka ngazi ya kituo kwa taarifa za chanjo kwa kutumia mtandao.
“Muhimu tuendelee kutoa chanjo kwa wote bila kukosa.
Tuzingatie mwongozo uliotolewa na Wizara wa kujilinda na Corona.” Alisema Richard Magodi.
Ambapo aliwataka watoa huduma hao kuhakikisha wanajilinda kwa kuvaa barakoa wakati wote pamoja na tahadhari zingine.
Aidha, akielezea hamasa ya chanjo ya HPV, aliwaagiza wasimamizi wa Zahanati, vituo kuhakikisha wanakaa na kamati za afya za maeneo yao ili kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka wasichana wa miaka 14 kupatiwa chanjo hiyo.
“Chanjo ya HPV tunaamini shule zimefungwa watoto wako majumbani hivyo mkae na kamati za afya za kituo, uongozi wa vijiji na kuendelea kuhamasisha kupitia nyumba za ibada ili watoto wasichana wa miaka 14 wajitokeze kupatiwa chanjo” alimalizia Richard Magodi.
Ziara hiyo ya kukagua utoaji wa huduma za Chanjo mkoani hapa inaendeshwa na Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD) kwa kushirikiana na wadua wake Shirika la Engender Health kupitia Meck Sharp & Dohme B.V (MSD).
Katika ziara hiyo pia imeshuhudiwa watoa huduma za chanjo wakiendelea na majukumu yao ambapo vifaa kama ndoo za maji, sabuni na alama za kupishana mtu na mtu ilikujikinga na virusi hivyo vya Corona.