Home Mchanganyiko KESI 6 KATI YA 30 ZA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA ZIMERIPOTIWA KITUO CHA...

KESI 6 KATI YA 30 ZA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA ZIMERIPOTIWA KITUO CHA POLISI WILAYANI WETE

0
***********************************

Na Masanja Mabula , Pemba.

JUMLA ya Kesi sita kati  ya 30 za udhalilishaji wa kijinsia zilizoripotiwa katika Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ndizo zilizofikishwa mahakamani kwa kipindi cha kuanzia mwezi wa Januari hadi Mei Mwaka huu.

Afisa Dawati kutoka Jeshi la Polisi Wete, Nadya Hilal Mfaume, alisema kati ya kesi hizo 20 zipo Polisi ambapo kesi nne zimefungwa.

Hayo aliyabainisha wakati akiwasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa vitendo hivyo kwa wajumbe wa mtandao wa kupinga udhalilishaji Wilaya hiyo.

Aidha alisema kuwa katika kipindi hicho kesi nyingi zilizoripotiwa  17 ni za ubakaji na  kesi za Kutorosha Msichana Saba ambapo shambulio la aibu  zimeripotiwa kesi nne.

Alieleza kuwa kesi hizo zilizoripotiwa katika kipindi hicho hakuna kesi iliyofikishwa mahakamani na kutolewa hukumu na wahusika kutiwa hatiani.

“Tumepokea kesi 30 kwa kipindi hichi  na kati ya hizo 20 zipo  Kiuto cha polisi nne zimefungwa na sita ziko mahakamani  changamoto kubwa ni wananchi kuendekeza rushwa muhali “alisema.

Kwa upande wake Rashid Hassan Mshamata, kutoka Jumuiya ya wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Wete alisema kati ya Kesi hizo Jumuiya hiyo imefanikiwa kushiriki kuibua kesi Kumi ambazo zinahusisha Ubakaji, Ulawiti utelekezaji, Ujauzito pamoja na Biashara ya Ngono.

“Jumuiya ya wasaidizi wa sheria kwa njia moja ama nyengine tumeshiriki kuziibua na bado tunaendelea kuzifuatilia kuona mwenendo wake”alisisitiza.

Katika kuhakikisha mtandao huo unazifuatilia kesi hizo pia mtandao umejumuisha wajumbe kutoka Wilaya ya Micheweni ambapo kumeripotiwa jumla ya kesi 12 na  kati ya kesi hizo Nne zinahusisha Mimba kwa wanafunzi wa Skuli za Msingi na Sekondari.

Kwa upande wake Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA, Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said aliwataka wajumbe wa mtandao huo kuendelea kuzifuatilia kesi hizo kwa ukaribu hasa katika kipindi hiki cha uwepo wa Virusi vya Corona.

Aliongeza kwa kuwataka kufanyakazi kwa ukaribu na waathirika wa vitendo vya udhalilishaji ili kuwahamasisha na kuwashawishi kujitokeza kutoa ushahidi Mahakamani pindi wanapohitajika.

“changamoto kubwa  ni jamii kujitokeza kwenda kutoa ushahidi, hivyo nashauri sana tuendelee kuihamaisha jamii ili iweze kushiriki kuyatokomeza matendo hayo kwa kutoa ushahidi”alisisitiza

Ripoti hizo ni utekelezaji wa Mradi wa Jukwaa la wanahabari la kumaliza vitendo vya udhalilishaji Zanzibar unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake – TAMWA, Zanzibar kwa ufadhili wa Danish International Development Agency (DANIDA)