…………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepongezwa kwa hatua zote alizochukuwa za kupambana na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi Corona ambapo amefanikiwa kulinda usalama na uhai wa Raia wake.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 20, 2020 na Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu kwenye mkutano na Wananchi uliofanyika Kijiji cha Ruvuma kilichopo kata ya Mihambwe wakati wa ziara ya kikazi ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mtwara Mark Samson Njera ambapo alisema jitihada za Rais Magufuli kupambana na Corona Watanzania wanajua na Dunia inajua pia.
“Kwa niaba ya Wakazi wa Tarafa ya Mihambwe tunampongeza na kumshukuru Rais Magufuli kutoa fedha, kulipa Madaktari, kulipia dawa pamoja na kutuondolea hofu nyakati zote za mapambano ya ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na kirusi Corona. Jitihada za Rais Magufuli zimeonekana toka hapa kijijini mpaka Dunia nzima wakajua tuna Rais Makini, mchapakazi, hodari na Mcha Mungu.” Alisema Gavana Shilatu.
Akizungumza mkutanoni hapo RPC Njera alisisitiza Wananchi kuendelea kuiunga mkono na kushirikiana na Serikali nyakati zote ili kudumisha amani na usalama.
“Hii ni ziara yangu ya Kwanza kabisa kutembelea Kijiji na kuongea na Wananchi tangu niteuliwe kuwa RPC. Nawaambieni Serikali hii inawajali, inawapenda. Tuendelee kulinda amani, tuendelee kushirikiana kwa pamoja.” Alisema RPC Njera.
RPC Njera amefanya ziara ya kikazi Tarafa ya Mihambwe kwa kuongea na viongozi mbalimbali, Wenyeviti wa vijiji, Watendaji kata, Watendaji wa vijiji, Afisa Tarafa na Askari wa Jeshi la akiba (Mgambo) na Polisi. Lengo la ziara hiyo ni kuweza kujitambulisha ikiwa ni pamoja na kuwataka viongozi wa Serikali na Wananchi kwa ujumla kushirikiana na Jeshi la Polisi kulinda usalama na kudumisha amani tuliyonayo.