………………………………………………………………………………………..
Na Masanja Mabula,Pemba.
JUMUIYA ya Kwanini Foundation imetoa vipima joto 12 na barakoa 3000 ,kwa ajili ya wakaazi wa shehia ya Tondooni na Makangale katika Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba ,ili kusaidia kuwakinga wananchi dhidi ya maambukuzi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19.
Afisa Jinsia wa Jumuiya ya Kwanini Foundation Rabia Rashid alisema wameamua kutoa msaada huo wa vipima joto na Barakoa ili kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID 19.
Alisema barakoa hizo zitagawiwa kwa wakaazi wa shehia ya Tondooni na Makangale na kuwataka kuzitumia kama lengo lililokusudiwa.
“Tumeamua kuungana na serikali kwa kutoa vipima joto 12 pamoja na barakoa 3000, lengo ni kuwakinga wananchi dhidi ya virusi vya Corona”alifahamisha.
Msaidizi Mkurugenzi maswala ya Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Mohammed Nassor Khamis alisema Kwanini Foundation wamefanya jambo la maana kutoa msaada huo kwani utasaidia kuwalinda wananchi na virusi vya Corona.
Alisema kinga ya virusi hivyo ni kutumia barakoa kwani asilimia kubwa ya maambukizi yanatokana na uwepo wa mikusanyiko ya watu.
“Hizi barakoa zitasaidia kuwakinga wananchi dhidi ya irusi vya Corona ,wakati hivi vipima joto vitasaidia kutambua wenye maambukizi kwa wakati”alieleza.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Bi Salama Mbarouk Khatib alisema mkakati wa wilaya hiyo ni kuwapima wananchi wote ili kuweza kubaini wenye maambukizi na kuandaa utaratibu wa matibabu.
Mbali na kushukuru msaada huo, Mkuu huyo wa wilaya aliahidi kuendelea kuthamini na kutambua mchango wa Jumuiya hiyo kwani utasaidia mapambano dhidi ya Virusi vya Corona.
“Mkakati wa serikali ni kuwapima wananchi wote, hii itatusaidia kuweza kutoa huduma kwa watakaobainika kuwa na maambukizi ya virusi vinavyasababisha ugonjwa wa Covid 19”alisema.
Msaada huo umetajwa kusaidi kudhibiti ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona ambapo Msaidizi Mkuu wa msitu wa hifadhi wa serikai Ngezi Suleima Mhammed alisema watautumika kama lengo lililokusudiwa.
Vipima joto hivyo vimegawiwa kwenye vituo vya afya pamoja na sehemu zenye kupitisha watu ikiwemo kwenye lango la msitu wa hifadhi wa Ngezi.