*****************************
Na Masanja Mabula,PEMBA
‘HUJAFA hujaumbika’, hivo ndivyo unavyoweza kusema na hakika matatizo yameumbiwa binadamu.
Je, ulishawahi kujiuliza kwamba wakati wewe au familia yako mmejaaliwa uwezo wa kula milo mitatu na kwa wakati , kulala sehemu nzuri, kunywa na kusaza lakini wapo wengine ambao kula na kulala yao ni kama hadithi za kusadikika.?
Ni majira yapata saa Nne na nusu Asubuhi, nilifunga safari hadi Kijiji cha Mbayayani, Shehia ya Kiwani Wilaya ya Mkoani Kusini Pemba na kupiga hodi Nyumbani kwa Mzee Haji Jeilan Alei (71) ambae ni Baba mlezi wa Bi Asha Rajab Shaaban (26) mlemavu wa miguu ambae pia ni mwathirika wa vitendo vya udhalilishaji aina ya utelekezaji.
Mzee Alei anaishi yeye na mwanae huyo mlemavu pamoja na wajukuu zake watatu. Na licha ya hali duni ya maisha wanayokabiliana nayo lakini tabasamu na ucheshi ndiyo alama ya nyuso zao wakati wote uwaonapo.
Bi Asha Rajab Shaaban alizaliwa ni mzima lakini alipata ulemavu wa miguu baada ya kuingia kwenye ndoa na kujifungua mtoto wake wa Pili mwaka 2016.
“Nilizaliwa ni mzima natembea vizuri hadi nikabahatika kupata mume, lakini baada ya kuolewa nilijifungua mtoto wangu wa kwanza salama. Nilianza kupata matatizo baada ya kujifungua mtoto wangu wa Pili ….Alisema Asha.
Licha ya kukumbwa na mtihani huo akiwa katika ndoa yake lakini alikumbwa na mtihani mwingine zaidi wa kutelekezwa na mume wake kwani baada ya kupata ulemavu mume wake aliamua kuoa mke mwingine na kusitisha hudumia pasipo kujali tatizo lake la ulemavu.
“Baada ya kujifungua na kuanza kupatwa na matatizo mume wangu aliamua kuoa mke mwingine akamleta katika nyumba yangu, nikawa nakosa huduma ndio nikaamua nirudi nyumbani, alisema huku akionesha sura ya huzuni.
KUHUSHU SHUGHULI
Kuhusu kujishughulisha, Asha alisema kabla ya kupatwa na ulemavu alikuwa akijishushulisha na ufumaji wa Mikoba ya ukili lakini baada ya kupatwa na matatizo alisitisha kutokana na kukosa uwezo wa kwenda kupakasa ukili.
“Nimeshaomba sana msaada wa Kigari ili niweze kutembelea kwaajili ya kuendelea na shughuli ndogo ndogo lakini hadi leo sijapata na maisha yangu yanazidi kuwa magumu kutokana nimekuwa mtu wa kukaa tu na watoto wanahitaji huduma, alisema.
Aliongeza, “Wazazi wangu washakuwa watu wazima, na mimi mahudumikio yangu ni mengi sana, kuna maji na hapa maji nyapo mbali sana, utaftaji wa Sabuni, Chakula na Mavazi kwa watoto ni changamoto kubwa sana kwangu.”
“Naiomba angalau Serikali na mtu yeyote anayeweza kunisaidia japo nipate Kigari cha kutembelea pamoja na msaada wa kuniwezesha kuendelea na shughuli ndogo ndogo kwani maisha ni magumu sana Watoto wananiangalia mimi niwahudumie nguo za Skuli na chakula na hali yangu ndio kama unavyoiona nimekuwa mtu wa kushinda ndani tu,” alisema huku akigeukia chumba chake kilichotanda kiza kinene.
Sheha wa Shehia ya Kiwani Abdalla Makame Hamad, allisema baada ya mama huyo kutelekezwa na mume wake walichukua hatua za kuwa karibu na familia hiyo ku kusaidia kutoa baadhi ya huduma za msingi ili aweze kujikimu wakati taratibu za kufuatilia haki yake zikiendelea.
Nae Mratibu wa Wanawake na Watoto Shehia ya Kiwani, Mwanaid Vuale Khatib alisema tayari kesi yake imeripotiwa usitawi wa Jamii na wameahidi kwenda kumuona ili aweze kupata haki zake.
“Baada ya kuipata kesi hii tumeiripoti ofisi ya Usitawi wa Jamii ili waweze kuja na kuona ni kwa namna gani aweze kupata haki zake na kuondokana na huu udhalilishaji anaokabiliana nao,” alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar) Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said aliahidi kutafuta mbinu za kumsaidia ili aweze kuendelea na shughuli za kujipatia kipato na kuondokana na changamoto hiyo.
“Kutokana na hali aliyonayo Bi Asha na sisi kama TAMWA Zanzibar tumekuwa tukifanya kazi za kuwawezesha waathirika wa vitendo vya udhalilishaji hivyo tutaangalia ni kwanamna gani tuweze kumsaidia ili aweze kuendelea na shughuli zake,” alisema Fat-hiya.
Ni wazi kwamba ‘kabla hujafa hujaumbika’ na hakika Bi Asha Rajab Shaaban anahitaji msaada wako. Anaomba msaada wako kupitia Namba