Mkurugenzi wa Ufundi Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa akizungumza na Wanahabari leo katika maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambayo hufanyika Mei 20 kila mwaka.
***********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Wananchi wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo katika biashara kwa wanunuzi na wauzaji ili kuweza kufikia uchumi wa kati.
Ameyasema hayo leo Mkurugenzi wa Ufundi Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa katika maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Mei 20 ambapo maadhimisho ya mwaka huu kaulimbiu “VIPIMO KATIKA BIASHARA ZA KIMATAIFA”.
“Wadau wetu na watanzania kwa ujumla tuzingatie sana matumizi sahihi ya vipimo kwasababu kipimo ndo haki yako,kipimo ni kitu muhimu katika maisha yetu ya kila siku toka unapoamka asubuhi mpaka unapolala usiku utakuwa umetumia vipimo vya aina mbalimbali kulingana na mahitaji yako ya kila siku”. Amesema Bi.Stella.
Aidha Bi.Stella amesema kuwa Tanzania ya Viwanda inajengwa kwa kuzingatia vipimo sahihi kwa njia ya malighafi mpaka mali iliyozalishwa hivyo ili kuweza kuingia katika biashara ya ushindani tunatakiwa tuzingatie vipimo.
“Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinafanya biashara za kimataifa na nchi mbalimbali kwa kutoa bidhaa nchini kupeleka nje ya nchi pia kuna bidhaa zinatoka nje ya nchi zinaingia hapa nchini”.
Pamoja na hayo Bi.Stella ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kwa kiasi kikubwa kwani mpaka sasa wanamagari ya kutosha, watumishi wameongezwa pia wameweza kufanikiwa kupata kituo kikubwa kwaajili ya kupimia magari ya mafuta.