………………………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MKUU wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama ,amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha na timu yake kufunga hoja 18 zilizokuwa hazijafungwa kwa mwaka 2017/2018 na kufanyia kazi maelekezo ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG ),ndani ya wiki moja.
Aidha ametoa maagizo mengine makubwa manne kwa halmashauri hiyo ikiwemo kuepuka kuingia mikataba mibovu inayosababisha hasara baadae na kudhibiti vyanzo vya ndani vya mapato.
Akizungumza katika kikao cha madiwani na baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo ,kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ,Assumpter alieleza ,kuanzia sasa mtumishi atakae sababisha kutokufungwa kwa hoja awajibishwe bila kuonewa aibu .
Mkuu huyo wa wilaya ambae anakaimu mkuu wa mkoa wa Pwani ,alisema ,kuna hoja mbalimbali za kipindi cha nyuma ambazo hadi sasa hazijafanyiwa kazi ambapo zipo ndani ya uwezo wao.
“;Epukeni kuzalisha hoja na mzingatie kanuni za kudhibiti mapato na matumizi ili kukamilisha hoja za mkaguzi mkuu ;:
” Nawapongeza kwa kupata hati safi miaka mfululizo lakini endeleeni kusimamia mapato yenu ,na kubuni vyanzo vipya ili kuinua mapato ,kwa maslahi ya halmashauri na wana Kibaha “alifafanua Assumpter .
Assumpter aliwaagiza kubuni miradi mkakati mipya itakayokuwa na tija ya taswira ya mji huo kama walivyofanya katika soko na stendi .
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya ,aliwaelekeza kumteua mtumishi muadilifu katika kitengo cha awali kabla ya malipo .
” Chukueni hatua za kinidhamu kwa mtumishi anaesababisha hasara “;alisisitiza Assumpter.
Katika hatua nyingine ,aliitaka halmashauri hiyo kutilia mkazo suala la elimu .
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini ,Silvestry Koka aliomba ushirikiano uendelee na kudai wakati mji huo ukielekea katika manispaa ni lazima kujipanga kuupanua na kujiwekea mikakati madhubuti .
Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha ,Jennifer Omolo alisema amepokea maelekezo ya mkuu wa wilaya na watayafanyia kazi .