**************************
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
19.5.2020
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR -TAMISEMI) inatekeleza Mpango wa wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara (BLUE PRINT) unaolenga kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji kwa Njia ya Majadiliano ili kuwainua Wananchi Kiuchumi.
Mpango huo unatekelezwa ili ili kukabiliana na changamoto za kibiashara na uwekezaji hususani zinazokwamisha kukua kwa biashara na maendeleo ya kiuchumi katika ngazi ya chini na wananchi wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi Vijijini na Mijini.
Mpango unahamasisha uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji kwa vitendo ili kutatua changamoto za kibiashara ambazo Serikali inakabiliana nazo katika kukuza uchumi, kuleta maendeleo, kukuza ajira na kuondoa umasikini katika Taifa.
Katika kuhakikisha kuwa mpango huu unatekelezwa kikamilifu, wadau mbalimbali wameshirikishwa ambao ni Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, Ofisi ya Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Jumuiya ya Tawala za MitaaTanzania (ALAT), Chemba ya Wafanyabiashara, Wakulima na Wenye Viwanda Tanzania (TCCIA) na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF).
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo anasema Serikali inasimamia na kutekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara (BLUE PRINT) unaokusudia kuondoa vikwazo na kero mbalimbali za biashara na uwekezaji ili kurahisisha mazingira ya kufanyia biashara.
Anasema kufikia Februari 2020 tozo mbalimbali zimeondolewa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa zikiwemo ushuru wa huduma kwa biashara za nyumba za kulala wageni, marekebisho ya ushuru wa mazao kati ya asilimia 3 hadi 5 wa awali hadi asilimia 3 kwa mazao ya biashara na chakula yasiyopungua tani moja.
‘Tozo na ushuru huo umeondolewa kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017, aidha Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuondoa kodi zenye kero zinazokwamisha ufanyaji wa biashara na uwekezaji zikiwemo tozo zinazotozwa na Taasisi zaidi ya moja’’ anasema Waziri Jafo.
Waziri Jafo anasema hadi Februari 2020, jumla ya hekta 854,821.59 zimetengwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya uwekezaji zikiwemo hekta 403,784.92 kwa ajili ya viwanda vikubwa, vidogo na vya kati pamoja na hekta 45,231.33 zilizotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa masoko, minada, hoteli, ujenzi wa stendi za mabasi, maduka na biashara.
Akifafanua zaidi Jafo anasema kupitia kaulimbiu ya Mkoa Wetu, Viwanda Vyetu, iliyoanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/18, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imesimamia na kutoa hamasa kwa wadau na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mkakati wa ujenzi wa viwanda ili kukuza uchumi na ustawi wa jamii.
Anasema hadi kufikia Februari 2020, jumla ya , viwanda 4,876 vimeanzishwa na kuvuka lengo la kuanzisha viwanda 2,600 lililowekwa sawa na viwanda 100 katika kila Mkoa kwa Mikoa yote 26 Tanzania Bara, ambapo kati ya hivyo viwanda vikubwa ni 108, viwanda vya kati ni 236, viwanda vidogo 2,522 na viwanda vidogo sana 2,010.
Jafo anasema Mikoa 8 ya Tabora, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Geita, Songwe, Morogoro na Dodoma imefanikiwa kuandaa wasifu wa kiuchumi ili kubainisha fursa za kiuchumi na uwekezaji unaotumika kuandaa makongamano ya uwekezaji yanayotumika kuwatangazia wadau fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Mikoa hiyo ili waweze kuzitumia.
Kuhusu vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, Jafo anasema hadi Februari 2020, jumla ya wafanyabiashara wadogo 1,551,126 wamepatiwa vitambulisho ambavyo vimewezesha kukusanywa kwa Tsh. Bilioni 31.02 katika Mikoa yote 26, huku lengo kubwa likiwa ni kuwatambua wafanyabiashara wadogo na kuwawekea mazingira rafiki ya ufanyaji biashara.
‘Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa Kanuni za kusimamia wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wadogo ili kutambua mchango wa biashara hizo katika ukuaji wa uchumi’’ anasema Waziri Jafo.
Pia Jafo anasema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Utoaji wa Vibali vya Ujenzi ulioanza kutekelezwa mwaka 2018 kwenye Halmashauri 184 Tanzania Bara, ambapo mwongozo umesaidia kupunguza muda wa kushughulikia kibali cha ujenzi kutoka wastani wa siku 180 hadi wastani wa siku 7.
Kuanzishwa kwa Mpango wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara (BLUEPRINT) kutasaidia kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa vitendo na kubadilisha hali ya uchumi wa jamii, kupunguza gharama na vikwazo vya kibiashara na kuwa na msingi thabiti wa mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Aidha uwepo wa Mpango huo pia utafafsiri kwa vitendo Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Maendeleo Endelevu ya Kimkakati (SDGs) pamoja na na mikakati mbalimbali ya Serikali.