*****************************
Na Masanja Mabula,PEMBA
KATIBU Tawala Wilaya ya Chake Chake Omar Ali, amepongeza juhudi zinazochukuliwa na chama cha Waandishi wa Habari wanawake TAMWA, Zanzibar katika kusadia mapambano dhidi ya maambuki ya Virusi vya Corona katika Jamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo vilivyotolewa na chama hicho huko chake chake Mkoa wa Kusini Pemba, alisema Serikali imeridhishwa na mchango huo kwani utazisaidia jamii kujikinga na virusi hivyo.
Mratibu wa kupabana na Corona kutoka Wizara ya Afya Pemba, Dok. Khamis Bilali Ali, amesema kitendo cha TAMWA kutoa msaada huo na kuwapelekea wananchi vijijini itazisaidia jamii ambazo hazina uwezo wa kumudu kununua vifaa hivyo kujiweka katika mazingira salama.
” Ni jambo jema ambalo limefanywa na TAMWA, na kwamba serikali itaendelea kuthamini mchango wa taasisi binafsi katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona”alisema.
Awali mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Musa alisema TAMWA kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Afya katika mapambano dhidi ya CORONA chama hicho kimeamua kuchangia Barakoa na vitakasa Mikono ili visaidie jamii katika kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.
“TAMWA ni sehemu ya jamii hivyo tumeamua kutoa msaada huu kwa ajili ya kuikinga jamii dhidi y Ugonjwa wa COVID 19″alisema.
Halfa hiyo ni matokeo ya mwendelezo wa juhudi za TAMWA kuwawezesha wanawake kujiinua kiuchumi katika kipindi hiki cha uwepo wa mripuko wa virusi vya Corona ambapo Zaidi ya Shilingi Milioni 19 zimetumika Unguja na Pemba katika kufanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo.