**********************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
WAZIRI wa TAMISEMI ,alhaj Selemani Jafo ,hajaridhishwa na ujenzi wa halmashauri ya Chalinze ambao unasuasua tangu mwaka 2018 na kuagiza mkandarasi ambae ni Wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuondolewa baada ya mei 31 mwaka huu.
Amemuelekeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo na timu yake wahakikishe awamu ya kwanza ya ujenzi inapokwisha mwezi huu watafute mjenzi mwingine wa majengo hayo .
Jafo alitoa kauli hiyo ,wakati alipokwenda kukagua na kujionea kasi ya ujenzi wa majengo ya halmashauri ya Chalinze na halmashauri ya wilaya ya Kibaha pamoja na hospital ya wilaya ya halmashauri ya Kibaha iliyopo Mlandizi.
Alisema ,kasi ya ujenzi huo ni mbaya ,haiendani na fedha ya bilioni 1.8 ya awamu ya kwanza ya ujenzi kwani ilipaswa wawe wamemaliza japo ghorofa moja .
“Ujenzi huu upo barabarani hapa ,halileti picha nzuri kabisa ,maana tangu mwaka 2018 ni nondo tu ndio zinachomoza ,majengo hayaishi”;Hatuwezi kuvumilia utaratibu huu wa zimamoto ,inaonekana kazi Leo inafanyika baada ya kujua ujio huu ,hatuwezi kwenda na mwenendo huu”alisema Jafo.
Aidha alikemea tabia ya wataalaamu wa ujenzi ,wahandisi kutokuwa na taarifa sahihi za ujenzi ambapo yeye anapokwenda kukagua na kuuliza maswali anamaanisha na sio kuanza kutafutiwa taarifa .
” Sijaja kutembea hapa ,nahitaji maelezo ya mradi ,nikuuliza jengo lina mita za mraba ngapi nahitaji majibu na sio kuanza kutafutafuta na kutafuta taarifa katika makaratasi “;tuwe makini na kazi zetu “;hakuna wa kuwajibia kila mtu awajibike katika nafasi yake”
Nae mbunge wa Chalinze ,Ridhiwani Kikwete, alibainisha ifikie hatua tuache kufanya kazi kwa mazoea ,na tuheshimu fedha za umma kwa maslahi ya watanzania.
Meneja TBA mkoa wa Pwani ,Asha Muyanza alikiri kuchelewa kwa jengo ,lakini ni kutokana na ukosefu wa maji na gharama za vifaa ambavyo ilikuwa tofauti ambapo ujenzi ungekamilika mwaka 2018.
Kwa upande wake mhandisi wa halmashauri ya Chalinze, John Chizima alisema ujenzi ulipaswa ukamilike 2018 ,na gharama za ujenzi awamu ya kwanza ni bilioni 1.8 na hadi kukamilika kwa ghorofa tatu itagharimu kiasi cha sh .bilioni 5(tano ).
Baada ya kutembelea ujenzi huo alipata fursa ya kutembelea majengo ya ujenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Jafo ameridhishwa na ujenzi huo ambao utagharimu zaidi ya sh .bilioni nne .
Jafo alimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Butamo na timu yake wasimamie miradi ikiwemo mradi wa hospital ya wilaya ukamilike kwa wakati.