*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Shirika la viwango Tanzania TBS, limewataka wazalishaji wa umeme mdogo wa nishati mbadala kuhakikisha wanawaona TBS kwanza ili waweze kujiridhisha na kiwango cha uzalishaji umeme kama unakidhi viwango.
Akizungumza na mwanahabari wetu Jijini Dar es Salaam, Afisa Viwango upande wa uhandisi wa umeme TBS, Bi.Neema Msemwa amesema kuwa kama una mradi wako wa kuzalisha umeme kabla ya kuanza kuutumia unatakiwa kuwaona TBS kwaajili ya kujiridhisha kiwango cha uzalishaji wa umeme huo kama unakidhi viwango ili kuondokana na madhara yatakayojitokeza kwa mtumiaji.
“Watumiaji bidhaa hasa vifaa vya umeme wamekuwa wakipenda kununua bidhaa za bei rahisi na hawaangalii ubora uliopo katika bidhaa hizo pia kunaweza kumleta madhara makubwa ya gharama ya kununua bidhaa nyingi” Amesema Neema.
Aidha amewataka watumiaji wa betri za magari katika matumizi ya umeme majumbani ama katika shughuli zao za kiofisi wazihakiki kama ni salama kwa matumizi kwani kunaweza kuleta madhara makubwa
“Mtumiaji wa betri ya magari katika kuzalisha umeme anatakiwa awe na elimu,betri kitu ambacho ni hatari sana zile terminal za juu ya betri zikileta shoti ambayo inaweza kusababisha mlipuko”.Amesema Bi.Neema.
Aidha Bi.Neema amesema kuwa watumiaji wa mabetri ya magari wanatakiwa watumie mabetri imara pamoja na kuyaweka katika sehemu salama kwa kuyajengea ili kusiweze kuleta usumbufu na kusababisha kutokea kwa shoti na kulipuka.
Shirika hilo pia limewataka wadau wote hasa wafanyabiashara na wenye viwanda kuendelea kufuata utaratibu wa kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango ili kuweza kumlinda mtumiaji.