Home Mchanganyiko SHIA ITHNA ASHERIA MWANZA WAKABIDHI VIFAA KINGA VYA CORONA JESHI LA POLISI

SHIA ITHNA ASHERIA MWANZA WAKABIDHI VIFAA KINGA VYA CORONA JESHI LA POLISI

0
Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mission of Tanzania, tawi la Mwanza na Kanda ya Ziwa, Alhaji Sibtain Meghjee kwa niaba ya waumini wa Khoja  Shia Ithna Asheria jijini humu akimkabidhi Ofisa Mnadhimu wa Polisi, Safia Jongo (kulia) kwa niaba ya Kamanfa wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, msaada wa barakoa 300, sanitizer chupa 500 na vitakasa mikono 500 kwa ajili ya askari wa jeshi hilo kujikinga na virusi vya corona. 
(katikati) akiwa na baadhi ya maofisa wa polisi Mkoa wa Mwanza baada ya kukabidhi barakoa, vitakasa mikono na sanitizer kwa jeshi hilo juzi katika mapambano ya kujikinga na corona, msaada huo ulitolewa na waumini wa dhehebu la Khoja Shia Ithna Asheria la jijini humu.Picha zote na Baltazar Mashaka

………………………………………………………………………………………..

NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza

WAUMINI wa madhehebu ya Khoja Shia Ithna Asheria, jijini Mwanza wamejitosa kwenye mapambano ya vita dhidi ya Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Kirusi cha Corona (Covid-19) kwa kutoa msaada wa vifaa kinga vya ugonjwa huo kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza.

Vifaa kinga hivyo barakoa 300, vitakasa mikono 500 na chupa 500 za sanitizer vilikabidhiwa juzi  kwa Ofisa Mnadhimu wa jeshi hilo mkoani humu, Safia Jongo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jumanne Muliro.

Akikabidhi vifaa hivyo Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mission Of Tanzania tawi la Mwanza na Kanda ya Ziwa Alhaji Sibtain Meghjee kwa niaba ya uongozi wa kina mama na vijana wa msikiti huo wa Shia Ithna Asheria, alisema umetolewa ili kuunga mkono juhudi za serikali na kutambua mchango wa jeshi la polisi katika kuhakikisha wananhudumia wananchi wakiwa salama.

“Askari polisi ni wadau muhimu kwa sababu wanahudumia wananchi wengi hivyo kwa kutambua hilo tumeona vema msaada huu tuuelekeze kwao ili wanapowahudumia wananchi wawe na vifaa kinga kwa ajili ya usalama wa afya zao na jamii wanayoihudumia,”alisema Meghjee abaye pia ni Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, tawi la Tanzania.

Akipokea msaada huo, Jongo aliwashukuru waumini wa madhehebu ya Shia kwa msaada huo na kuomba wasisite kuwasaidia tena endapo fursa kama hiyo itapatikana ikizingatiwa ugonjwa wa corona ni janga la kidunia na akatoa rai kwa askari kuhakikisha wanautumia msaada huo vizuri kwa ajili ya kujilinda na kuchukua thadhari muda wote.
Waumini hao wa Shia Ithna Asheria wamekuwa wa kwanza jijini Mwanza kujitoa kutoa msaada wa vifaa kinga kwa ajili ya askari polisi kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona.