………………………………………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
WAUMINI wa madhehebu ya Khoja Shia Ithna Asheria, jijini Mwanza wamejitosa kwenye mapambano ya vita dhidi ya Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Kirusi cha Corona (Covid-19) kwa kutoa msaada wa vifaa kinga vya ugonjwa huo kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza.
Vifaa kinga hivyo barakoa 300, vitakasa mikono 500 na chupa 500 za sanitizer vilikabidhiwa juzi kwa Ofisa Mnadhimu wa jeshi hilo mkoani humu, Safia Jongo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Jumanne Muliro.
Akikabidhi vifaa hivyo Mwenyekiti wa Bilal Muslim Mission Of Tanzania tawi la Mwanza na Kanda ya Ziwa Alhaji Sibtain Meghjee kwa niaba ya uongozi wa kina mama na vijana wa msikiti huo wa Shia Ithna Asheria, alisema umetolewa ili kuunga mkono juhudi za serikali na kutambua mchango wa jeshi la polisi katika kuhakikisha wananhudumia wananchi wakiwa salama.
“Askari polisi ni wadau muhimu kwa sababu wanahudumia wananchi wengi hivyo kwa kutambua hilo tumeona vema msaada huu tuuelekeze kwao ili wanapowahudumia wananchi wawe na vifaa kinga kwa ajili ya usalama wa afya zao na jamii wanayoihudumia,”alisema Meghjee abaye pia ni Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation, tawi la Tanzania.