************************************
Na. WAMJW-Morogoro
Serikali imekanusha taarifa zilizotolewa na baadhi ya mitandao ya kijamii zinazosema kuwa watu 92 wamekufa mkoani kwa corona katika kipindi cha wiki moja iliyopita na kuzikwa kwenye makaburi ya Kola yaliyopo katika manispaa ya Morogoro
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mkoani hapa mara baada ya kutembelea eneo hilo la makaburi na kufanya uchunguzi wa kuyaona makaburi hayo kama yanavyotangazwa
“Kumekuwepo na taarifa zinazoashiria matumizi yasiyo sahihi ya kimtandao na hivyo kuleta taharuki kwa wakazi wa Morogoro,imefika hapa nijionee mwenyewe makaburi hayo 92,sijayaona hayo makaburi yaliyosemwa”.Alisema Prof. Makubi
Katika ziara hiyo Prof. Makubi aliweza kutembelea sehemu zote za makaburi hapo Kola , ikiwa pia kupata taarifa toka kwa vijana wachimba makaburi ambao wamekuwepo hapo zaidi ya mwaka.
Aidha, Mganga Mkuu wa Serikali, aliwaasa baadhi ya wananchi kuacha kupotosha jamii kwa taarifa za uongo kama kwamba wao wanafurahia vifo.
Naye Mtunzaji wa makaburi hayo ALLY KASOLE ambaye alihojiwa pia, alisema maneno hayo ni uvumi maana hajawahi kuona kuchimbwa makaburi ya idadi hiyo kwa kipindi hicho bali ni makaburi 6 tu (kwa sababu mbalimbali za vifo) kwa siku 5 zilizopita na hakuna maziko ya usiku yanayofanyika kwenye makaburi hayo ya Kola. Kauli hiyo ilisisitizwa pia na wachimbaji wegine wa makaburi ambao walikutwa hapo.
Prof. Makubi amewatahadharisha ndugu wa marehemu kuacha kufungua miili ya marehemu iliyokwisha kufungwa na wataalamu wa afya. Vilevile amewataka wananchi kuendelea kujikinga na ugonjwa huo, kwa kuacha misongamano, kuvaa barakoa pamoja na kuzingatia usafi wa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabani.
Pia aliwasisitiza watumishi wa Afya kuendelea kusimamamia uandaji wa maziko ya marehemu wote kwa kufuata utu na heshima ya binadamu kwa kushirikisha familia kwa karibu.