Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (kulia) akizungumza na timu ya vijana kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali la Empower Youth Prosperity ( EYP) la mkoani Mbeya na Shirika la Sustanable Environment Management Action (SEMA) la Singida ambao walikuwa wilayani humo jana kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona. Katikati ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Winfrida Funto.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na vijana hao wazalendo kutoka katika mashirika hayo. Kushoto ni Afisa Afya wa wilaya hiyo, Naftal Kilangiro.
Mdau wa mapambano dhidi ya Corona kutoka Taasisi ya Empower Youth Prosperity ( EYP) ya mkoani Mbeya, Ipyana Mwakyusa akitoa elimu ya kujikinga dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Mdau wa mapambano dhidi ya Corona kutoka Taasisi ya Empower Youth Prosperity ( EYP) ya mkoani Mbeya, Amani Twaha, akitoa elimu ya kujikinga dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Afisa wa Shirika SEMA, Veronica Peter akionesha namna ya kunawa kwa usahihi kwa wakazi wa Ikungi.
Mdau wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona kutoka Shirika la EYP la mkoani Mbeya, Amani Twaha, akitoa maelekezo ya watu kukaa umbali wa mita moja baina ya mtu na mtu ili kuepuka kuambukizana virusi vya corona kama itatokea mmoja kati yao atakuwa na virusi vya Corona.
Afisa wa Shirika SEMA, Daria John akitoa elimu kwa njia ya bango kwa Mzee Petro Njiku wa Kijiji cha Matongo.
Mkazi wa Kijiji cha Matongo, Mohamed Hamisi, akionesha namna ya kunawa mikono baada ya kupata elimu.
Elimu kwa njia ya mabango ikitolewa Kijiji cha Matongo.
Mwanafunzi wa Darasa la tatu wa Shule ya Msingi ya Nkhoire, Christina Isack akionesha namna ya kunawa mikono kwa usahihi baada ya kupata elimu.
Afisa Mradi toka Shirika la SEMA, Nice Daudi, akizungumza na wananchi wa Kata ya Iseke kuhusu ugonjwa wa Corona.
Afisa wa Shirika SEMA, Gerson Janga akionesha namna ya kunawa kwa usahihi kwa wakazi wa Kata ya Iseke.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Iseke, Loveness Msigwa (kushoto) akinawa kwa usahihi baada ya kupata elimu.
Afisa Vijana Wilaya ya Ikungi, Samwel John, akizungumza na wananchi wa Kata ya Ihanja.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Ihanja, Juma Kisuda akielezea mafanikio ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.
Afisa wa Shirika SEMA, Witness Anderson akionesha namna ya kunawa kwa usahihi kwa Wauguzi na Madaktari wa Kituo cha Afya cha Ihanja.
Mdau wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona kutoka Shirika la EYP la mkoani Mbeya, Ipyana Mwakyusa, akitoa maelekezo ya watu kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu ili kuepuka kuambukizana virusi vya corona kama itatokea mmoja kati yao kuwa navyo katika Gulio la mji wa Puma.
Kampeni ya utoaji elimu kwa njia ya mabango ikifanyika. Kushoto ni Mary Kilimba kutoka SEMA na Kulia ni Veronica Peter.
Mwanasheria wa Shirika la SEMA, Joseph Lakati, akielekeza jambo katika Gulio la Ikungi.
Mdau wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona kutoka Taasisi ya Empower Youth Prosperity ( EYP) ya mkoani Mbeya, Ipyana Mwakyusa, akitoa elimu ya kujikinga dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona kwa Wananchi walikuwa kwenye Gulio wilayani Ikungi.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo ameyapongeza Mashirika yasiyo ya Kiserikali la Empower Youth Prosperity
( EYP) la mkoani Mbeya na Shirika la Sustanable Environment Management Action (SEMA) la Singida kwa hatua waliochukua ya kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kupambana na ugonjwa wa Corona.
Mashirika hayo kwa pamoja yamekuwa yakishirikiana kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.
Akizungumza jana na timu ya vijana kutoka katika mashirika hayo ambao walikuwa wilayani humo kutoa elimu hiyo, Mpogolo aliwapongeza kwa kuwa wazalendo na kujitoa kwa dhati kuisaidia Serikali kukabiliana na jambo hilo.
“Nawapongeza sana kwa kazi hii kubwa mnayoifanya na hasa nyie mliotoka Mbeya kwani nchi hii ina vijana wengi lakini hawafanyi kama mnavyofanya ninyi katika kuisaidia Serikali” alisema Mpogolo.
Mpogolo alisema Rais Magufuli katika kupambana na ugonjwa huu hakutaka kuwazuia wananchi kutoka majumbani mwao kama zilivyofanya nchi nyingine badala yake aliwataka watanzania waendelee kuchapa kazi huku wakichukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.
“Sisi hapa Ikungi tunalima sana viazi na kama Rais angetuzuia tusitoke sijui ingekuwaje kwani maeneo mengi yangekosa viazi hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani” alisema Mpogolo.
Vijana hao kutoka Shirika la SEMA kwa kushirikiana na wenzao kutoka Mbeya katika wilaya hiyo walifanikiwa kutoa elimu hiyo kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Kituo cha Polisi, Stendi ya Mabasi na maeneo mengine ya mji wa Ikungi.
Maeneo mengine waliotoa elimu hiyo ni katika Kijiji cha Matongo, Kata ya Iseke, Ihanja na kwa wananchi waliokuwa katika Gulio la mji wa Puma na Ikungi.
Mdau wa mapambano dhidi ya Corona kutoka Taasisi ya EYP ya mkoani Mbeya, Ipyana Mwakyusa alisema elimu wanayoitoa imelenga kukumbushana tu kwani kila mtu anajua uwepo wa ugonjwa wa Corona.
Afisa Mradi wa Shirika la SEMA, Renard Mwasambili alisema kampeni ya utoaji wa elimu hiyo mkoani hapa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo katika baadhi ya maeneo.
Meneja wa Shirika la SEMA, Ivo Manyaku alisema kampeni hiyo inafanywa kwa ufadhili wa Shirika la Stromme East Africa Foundation lenye Makao Makuu Kampala nchini Uganda kwa kushirikiana na Shirika la Stromme Foundation la Norway pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) kupitia mradi wa uwezeshaji jamii kiuchumi unaowalenga vijana.wa kiume, wa kike, watoto na wakina mama.