Wadau na wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, baada ya kumkabidhi ndoo 30 za kunawa mikono na vitakasa mikono lita tano za thamani ya shilingi 531,000 kwa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Paulo Bura kwenye kituo cha afya Katesh jana.
……………………………………………………………..
JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, kupitia kampeni yao ya mikono safi Hanang’ salama wameikabidhi serikali vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona vya thamani ya sh. 531,000.
Makamu Mwenyekiti wa kampeni ya mikono safi Hanang’ Emmanuel Gamasa akizungumza jana alisema lengo la UVCCM wilayani humo kukabidhi msaada huo wa vifaaa hivyo ni kuiunga mkono serikali katika mapambano ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Gamasa alisema wao kama UVCCM wilayani humo kupitia kampeni ya mikono safi Hanang’ salama wametoa vifaa hivyo vya kujikinga na corona kwa thamani ya sh. 531,000 kwa ajili ya wananchi wa eneo hilo kutumia.
Alisema wametoa ndoo 30 za kunawa mikono na vitakasa mikono lita tano ili kuiunga mkono serikali katika mapambano hayo dhidi ya corona.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ Dk Boniface Manditi aliwashukuru UVCCM wilaya ya Hanang’ kwa kuona uhitaji wa kujikinga na kuweza kuwajali wahitaji.
Dk Manditi alisema tahadhari zinazochukuliwa ni za muhimu kuliko hatua za kufunga mipaka, hivyo watu waendelee kunawa mikono kwa maji tiririka kwa sabuni, kuvaa barakoa na kufanya kazi.
”Hivi mlivyotusaidia leo tunashukuru sana na itaendelea kutuweka katika sehemu nzuri ya mapambano dhidi ya janga hili corona,” alisema Dk Manditi.
Katibu Tawala wa wilaya ya Hanang’ Paulo Bura baada ya kupokea msaada huo aliwashukuru UVCCM na kusema ni mfano wa kuigwa kwani bado kuna uhitaji wa vifaa hivyo.
”Siyo kuwa vijana wana fedha ila wakaona waguse kile kidogo walichonacho ili kufanikisha jukumu hili muhimu la kuunga mkono serikali yao katika mapambano ya janga hili la corona,” alisema Bura.
Aliwahakikishia vijana hao kuwa serikali ipo pamoja nao bega kwa bega na juhudi wanazozifanya kama UVCCM wanazitambua na vifaa walivyotoa vitatumika kwa makusudi yaliyokusudiwa.
”Vifaa hivi tunavikabidhi kituo cha afya cha Katesh ni imani yangu wataalamu wataangalia maeneo yote muhimu na kuweka ili ziweze kuwasaidia wananchi walio wengi, matarajio ya matunda na matokeo ya vifaa hivi yaweze kuonekana,” alisema Bura.
Mwenyekiti wa kamati ya uhamasishaji na maafa wa UVCCM mkoani Manyara, mwalimu Carol Gisimoy alisema hiyo ni awamu ya kwanza ya kumuunga mkono Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya janga la corona.
Mwalimu Gisimoy alisema UVCCM Hanang’ wametekeleza maelezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally ya kuitaka jumuiya hiyo kusimama mstari wa mbele kutoa elimu na tahadhari zinazoelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
Hata hivyo, aliwapongeza vijana wote walioshiriki shughuli hiyo na wadau wengine bila kuwasahau madaktari na wauguzi wanaokesha kuhakikisha jamii inaendelea kuwa salama.