Naibu Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akipitia taarifa ya ujenzi wa Hosteli za wanachuo wa kike wa Chuo Kikuu Mzumbe iliyowasilishwa alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Kampasi Kuu Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe (kushoto) akiwa ameambatana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Kusiluka, akikagua mradi wa ujenzi wa madarasa na kumbi za mihadhara wa chuo kikuu Mzumbe. Kulia ni Msimamizi wa mradi huo toka Kampuni ya SUMA JKT, Injinia Raymond Kweka.
Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa hosteli Injinia Issa Kanyaga akiwasilisha taarifa ya mradi wa ujenzi wa Hosteli za chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu, kwa Naibu Katibu
Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi leo.
Hapa Naibu Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa hosteli eneo la Maekani Kampasi Kuu Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe (kushoto) akiwa ameambatana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akipokea maelezo kuhusu maendeleo ya ujenzi kutoka kwa msimamizi wa mradi huo.
*******************************
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe, ametembelea na kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi
Kuu Morogoro, ambayo ni ujenzi wa hosteli za wanafunzi pamoja na ujenzi wa jengo la madarasa na kumbi za mihadhara.
Pamoja na kupongeza hatua nzuri ya maendeleo ya miradi hiyo; hakuridhishwa na kasi ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi kutokana na mradi huo kuchelewa kukamili kwa mujibu wa mkataba ambapo majengo hayo yalipaswa kuwa yamekamilika Desemba, 2019.
Amemtaka Mkandarasi kampuni ya Suma JKT, pamoja na changamoto zilizopo, kuhakikisha mradi huo unakamilika katika kipindi cha nyongeza alichopewa, ili majengo hayo kuanza kutumika katika mwaka ujao wa masomo.
Akizungumza wakati akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka amesema hadi Mei, 2020 ujenzi wa Hosteli za wanafunzi umekamilika kwa asilimia 86%, wakati ujenzi wa madarasa umefikia asiliamia 60%, na kwamba Chuo kinatazamia majengo hayo kuanza kutumika katika mwaka ujao wa masomo 2020/2021.
Akielezea sababu za kuchelewa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa hosteli, Msimamizi wa mradi toka Suma JKT Injinia issa Kanyaga, amezitaja sababu za kuchelewa kukamilisha mradi kuwa ni pamoja na uwepo wa ugonjwa wa Corona ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa kuweka vibarua wengi kwa wakati mmoja pamoja na upatikanaji wa baadhi ya malighafi hususani zile zinazoagizwa nje ya nchi.
Changamoto nyingine ni mabadiliko ya hali ya hewa yaliyoathiri miundombinu hususani barabara. Hata hivyo ameahidi kuhakikisha ujenzi wa hosteli hizo unakamilika kwa wakati kulingana na muda walioongezewa kwenye mkataba.
Naibu Katibu Mkuu, amehitimisha ziara yake kwa kukagua ghala ya kuhifadhi vifaa (malighafi) kujiridhisha kuwepo vifaa vya kutosha kumaliza kazi ya ujenzi iliyobaki, pamoja
na kukagua ubora wa majengo kwa sehemu zilizokamilika ikiwemo michoro ya ujenzi.
Ujenzi wa Hosteli unafadhiliwa na Serikali kwa kiasi cha TZS Bil. 6.5 na ulitazamiwa kukamilika mwezi Desemba 2019.