Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe akipokea msaada wa vifaakinga kutoka kwa Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe na Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke wakionyesha hati ya makabidhiano baada ya kutia saini kila mmoja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe akizungumza kabla ya kupokea msaada wa vifaakinga kutoka kwa Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Gabriel Mhidze akieleza jinsi msaada huo utakavyotumika baada ya kuupokea kutoka Serikali ya China.
*******************************
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea msaada wa vifaa kinga vyenye thamani ya Yuan 2,150,00 sawa na shilingi 700,759,268 kutoka Serikali ya China.
Msaada huo umetoleowa leo katika Bohari ya Dawa (Medical Stores Department) na kupokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Mabula Mchembe.
Prof. Mchembe amesema kwamba msaada huo umekuja wakati mzuri kwani utawasaidia watumishi wa afya katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19).
“Niwaombe na niwasisitize wafanyakazi wa afya, mjitahidi kuwahudumia watu wenye magonjwa mengine tofauti na ugonjwa wa Corona, huku mkiendelea kutekeleza wajibu wetu kwa wagonjwa wa Covid-19.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Gabriel Mhidze ameishukuru kwa kupatiwa msaada huo kutoka China na ameahidi kwamba utasambazwa kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.
“Nashukuru Serikali ya China kwa msaada huu, hivi sasa naweza kusema bohari yangu ina vifaa vya kutosha kusambaza kwa walengwa wote nchini,” amesema.
Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke amesema Serikali yake ya China imetoa barakoa 12,000, gloves 10,000, viatu 10,000 pamoja na vifaa kinga mbalimbali kwa ajili ya wataalamu wa afya.
“Ni matumaini yangu kwamba msaada huu ambao tumeotoa leo, utasambazwa kwa watalamu wa afya ili wavitumie wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa Corona na hivyo kuokoa maisha yao,” amesema.
Balozi Wang Ke.
Balozi huyo amemshukuru Rais John Pombe Magufuli pamoja na Serikali yake kwa msaada mkubwa iliyotoa kwa raia wa China baada ya kuibuka kwa janga la ugonjwa Covid-19 na hivyo kuleta nguvu ya pamoja katika kukabiliana na ugonjwa huu.
“Kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na janga hili la ugonjwa Corona, ili kulinda maisha ya watu wake, napenda kusema kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika mapambano haya,” amesema Balozi Wang Ke.
Amesema China na Afrika zinapaswa kuendelea kushirikiana katika kupambana na ugonjwa wa Corona, huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kutoa ushirikiano katika janga hili.