****************************
KUPATIKANA NA UNGA UDHANIWAO KUWA NI DAWA ZA
KULEVYA [HEROINE].
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia MPALUKA NYAGALI MDUDE [32] Mkazi wa Itezi Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na Unga unaodhaniwa
kuwa ni dawa za kulevya aina ya Heroine.
Kufuatia taarifa za ki-intelijensia zilizopatikana mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 10.05.2020 majira ya saa 17:00 Jioni katika msako uliofanyika huko
maeneo ya Kadege Stendi, Kata ya Forest, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya.
Mara baada ya kukamatwa mtuhumiwa Polisi walikwenda nyumbani kwake Mtaa wa Mwasote – Itezi Jijini Mbeya kwa ajili ya kufanya upekuzi na katika upekuzi
huo kulikutwa busta tano [05] za unga udhaniwao kuwa dawa za kulevya aina ya Heroine wenye uzito wa gram 23.4 ambao ulikuwa umehifadhiwa kwenye mfuko
wa kaki ambao ndani yake kulikuwa na mifuko midogo miwili ya Nylon.
Mtuhumiwa pia alikutwa na simu mbili za mkononi aina ya Samsung na Nokia, CD 24 za aina mbalimbali.
Mnamo tarehe 12.05.2020 unga huo udhaniwao kuwa dawa za kulevya ulipelekwa Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
kwa uchunguzi zaidi wa kimaabara na ilithibitika kuwa unga huo ni dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride wenye uzito wa gram 23.4.
Aidha ameelezwa kuwa, Heroine Hydrochloride husababisha ulevi usioponyeka kirahisi [Drug dependence] na hatimae husababisha mtumiaji kuharibikiwa na akili
na kwamba Dawa hizi pia zimo kwenye kundi la kwanza la orodha za sumu [Part One Poison].
Mtuhumiwa MPALUKA NYAGALI MDUDE pia alikuwa anatafutwa kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Serikali
ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania iliyopo madarakani ya awamu ya tano.
Upelelezi wa shauri hili unaendelea, mtuhumiwa amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.
WITO WA KAMANDA.
Ninatoa wito kwa wananchi kuacha matumizi ya dawa za kulevya kwani ni hatari kwa afya zao kwani mtumiaji wa dawa hizo anaweza kusababishiwa ulevi usioponyeka kirahisi [Drug dependence] na hatimae kuharibikiwa na akili.
Pia matumizi ya dawa za kulevya ni kinyume na sheria ya udhibiti, utumiaji na usafirishaji wa dawa za kulevya ya mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara.
Aidha ninatoa rai kwa wananchi kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya kwani Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yeyote atakaye kwenda kinyume na sheria zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.