Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha Unga wa sembe wenye viini lishe cha AMP Super Sembe, Alfred Mpanga akizungumza kuhusu uzalishaji wa unga wenye viini lishe unaosaidia jamii kupambana na udumavu na utapiamlo
Afisa Lishe wa Mkoa wa Iringa, Neema Mtekwa akizungumza na wanahabari hawapo pichani katika mahojiano maaluma kuhusu hali ya lishe mkoa wa Iringa. (Picha na denis Mlowe)
………………………………………………..
NA DENIS MLOWE,IRINGA
LISHE duni kutokana na wananchi kutokuwa na elimu ya ulaji wa vyakula vya kutosha na vyenye mchanganyiko wa viini lishe ndio sababu kubwa ya mkoa wa Iringa kuwa moja ya mikoa inayoongoza kwa watoto kuwa na utapiamlo na udumavu.
Akizungumza na wanahabari Afisa Lishe wa Mkoa wa Iringa, Neema Mtekwa alisema kuwa jamii imekuwa ikishindwa kutumia lishe yenye virutubishi hali inayosababisha kwa kiasi kikubwa kuwa na utapiamlo na udumavu licha ya mkoa wa Iringa kuwa moja ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji.
Alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2018 juu ya hali ya lishe nchini mkoa wa Iringa ina watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu 15,000 sawa na asilimia 47 huku kitaifa ikiwa na asilimia 31.8 huku watoto wenye ukondefu ni 8473 sawa na asilimia 3.7 huku kitaifa ni asilimia 3.8 na hali ya kuzaliwa na uzito pungufu ni asilimia 6.2 sawa na watoto 4842 kitaifa mkoa una asilimia 6.3.
Mkweta aliongeza kuwa uzito pungufu ni asilimia 18.4 sawa na watu 29,696 huku kitaifa mkoa ukiwa na asilimia 14.7 na uzito uliozidi ni watoto watoto 4842 sawa na asilimia 3 huku kitaifa ni asilimia 2.8.
Alisema kuwa sababu kubwa inazosababisha hali hiyo ni kutowekeza muda wa kuwa na watoto kuwalisha ipasavyo ikiwepo kuwapa pombe kwa baadhi ya maeneo, lishe duni kutokana na wananchi kutokuwa na elimu ya ulaji wa chakula cha kutosha na chenye mchanganyiko wa viini lishe.
Aliongeza kuwa visababishi vingine ni watoto wa miezi 6 hadi 23 wanaopewa kiwango cha chakula kinachokubalika ni asilimia 12 tu huku watoto hao wanaopewa mlo wenye mchanganyiko wa vyakula tofautitofauti zikiwemo mbogamboga, matunda na vyakula vyenye jamii ya kunde na nyama ni asilimia 25.
Alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo mkoa wa Iringa umeweka mikakati mbalimbali katika kuweza kupambana na hali ya utapiamlo na udumavu kwa watoto wenye chini ya miaka mitano ikiwemo kutoa elimu kwa jamii ya nadharia na vitendo kuhakikisha kwamba ulaji wa kiwango cha juu cha virutubishi unafanyika na kuzingatia unyonyeshaji katika siku 1000 za mtoto unafatwa.
Alisema kuwa mkoa wa Iringa katika kupambana na hali hiyo umekuwa ukishirikiana sekta mtambuka na wadau mbalimbali katika kutoa elimu juu ya lishe bora licha ya changamoto ya uhaba wa maafisa lishe lakini kupitia watoa huduma za afya jinsi gani ya kutoa ushauri wanasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu hiyo.
Alisema kuwa mkakati mwingine ni kuhakikisha halmashauri zote za mkoa zinatenga fedha za utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe kama kununua vyakula dawa , kutoa elimu za lishe, kupanga mipango ya lishe, kufanya siku za afya na lishe ya kijiji na mitaa hivyo mkoa unasimamia na halmashauri kutekeleza hayo.
Wakizungumza kuhusu changamoto hiyo baadhi ya wadau wanaozalisha unga wenye viini lishe mkoani hapa walisema kuwa mkakati moja wapo ni kuzalisha unga wenye viini lishe kwa ajili ya matumizi ya kila siku kwa jamii.
Mmoja wa wadau hao Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha Unga wa sembe wenye viini lishe cha AMP Super Sembe, Alfred Mpanga alisema kuwa walipewa mkakati wa kuzalisha unga wenye viini lishe kutoka kwa aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza kwa lengo la kupambana na udumavu na utapiamlo.
Alisema kuwa kutokana na hilo unga unaozalishwa kwenye kiwanda hicho lazima uwe na viini lishe ambavyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kupambana na udumavu na utapiamlo hali ambayo kwa kiasi kikubwa umesaidia kwa kiasi kikubwa jamii kubadilika.