…………………………………………………………………..
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amethibitisha kuingia kwa Sukari tani 90 kufuatia kupanda kwa bei ya sukari katika Wialaya ya Morogoro.
Hayo ameyazungumza Mei 11, 2020 Ofisini kwake katika kikao cha waandishi wa habari juu ya suala la kupanda kwa bei ya Sukari katika Wilaya ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Chonjo, amesema suala la Sukari limekuwa changamoto sana na sio Wilaya ya Morogoro hata Mkoa Mzima wa Morogoro sukari imekuwa tatizo.
Chonjo, amesema kupanda kwa sukari kumetokana na baadhi ya wafanyabiashara kuuza bei ya Sukari kinyume na bei elekezi ya Sukari iliyotolewa kupitia Bodo ya Sukari Tanzania.
Amesema kuwa anaishukuru Serikali kwa kushusha tani 90 kwa wafanyabiashara wakubwa ambapo wafanyabaishara hao wataisambaza sukari hiyo kwa wafanyabaishara wa nusu jumla kwa kufuata utaratibu ambao Serikali imeuweka.
“Upatikanaji wa Sukari hapa Wilaya ya Morogoro umekuwa changamoto kidogo, lakini sio Wilaya ya Morogoro tu na mkoa mazima pia , niishukuru Serikali ya Jamhuri hii ya awamu ya inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwa sikivu imeendela kutoa vibali ili tuweze kuagiza Sukari kutoka nje, na leo tumepokea Sukari tani 90 ambapo mgao wake utatolewa kwa wafanyabiashara wa jumla “ Amesema DC Chonjo.
Aidha amesema miongoni mwa wafanyabiashara wajumla ambao wamegawia Sukari hiyo kwa ajili ya kusambaza,ni pamoja na Sadiki amepata tani 30, Binzoo tani 30na Digamba tani 30.
Amesema Sukari hiyo itagaiwa kwa Mkoa mzima wa Morogoro na sio kwa Wilaya ya Morogoro peke yake
Amesema katika ugawaji huo kutokana na magari makubwa hayaruhusiwi kuingia mjini, hivyo ugawaji wake utafanyika maeneo ya maegesho ya magari Nane nane kwa kuwakabidhi wafanyabishara wa jumla tu ambapo baada ya hapo wale wajumla watasambaza kwa wafanyabiashara wa nusu jumla kwenye maduka yao ili kuepusha msongamano wa watu hususani katika kipindi hiki cha mapambano dhid ya Ugonjwa wa CORONA.
Kuhusu bei elekezi, Chonjo, amesema kwa wafanyabiashara wa jumla watatakiwa kuuza sukari hiyo kwa mfuko mmoja wa Kilo 50 kwa shilingi 127,000/= , kwa wale wanusu jumla watauza kwa shilingi 128,000/=na wale wa wafanyabiashara wa reja reja watatakiuwa kuuza kilo moja kwa shilingi 2,700/= kama bei elekezi inavyotaka.
Amesema wale watakao kiuka bei elekezi watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo kuwapa kesi ya uhujumu uchumi kwa kutakataa na kukiuka maagizo ya Serikali.
Mwisho amewaomba Wananchi wa Wilaya ya Morogoro kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito kwani suala la sukari litamalizika na kila mwananchi atanufaika na huduma hiyo na kurudi kama zamani kwani hata sukari iliyoletwa haiwezi kukidhi kwa maeneo yote hivyo wanatarajia kupokea tani nyeninge za siukari kutoka Serikalini.