Msimamizi wa mradi wa nyumba za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mhandisi Ali Shanjirwa (kushoto) akitoa maelezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio (katikati) kuhusu mradi wa nyumba hizo zilizopo Dungu, Kigamboni. Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji, Augustine Paul na Benedicto Mahela ambaye ni Meneja Manunuzi wa NSSF.
*******************************
Na MWANDISHI WETU
WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa ya nyumba za Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili waweze kuishi kwenye makazi bora na kwa bei nafuu.
NSSF imesema nyumba hizo 99 zote zipo Dungu, Kigamboni, Dar es Salaam, na tayari zimekamilika, ambapo nyumba 55 zimepangishwa kwa wananchi mbalimbali, nyumba 10 zimekabidhiwa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kigamboni na 16 zimekabidhiwa kwa wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Kigamboni.
Akizungumza wakati alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, amesema nyumba 15 zilizobaki zinapangishwa kwa wananchi mbalimbali wenye uhitaji kwa bei nafuu.
“Nawaomba Watanzania kuchangamkia fursa ya uwepo wa nyumba hizi ambazo zinauzwa na kupangishwa ili waishi kwenye makazi bora ambayo NSSF inayatoa,” amesema Erio.
Amesema mradi wa nyumba hizo umeshakamilika tangu mwishoni mwa mwaka jana, kufuatia maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Nyumba hizi ni mzuri kama mnavyoziona wenyewe hapa, hivyo kila mwananchi anayejitaji kupanga anakaribishwa,” amesema.
Erio alifafanua kuwa bei ya upangaji wa nyumba hizo ambayo imepitishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali kodi ni kati ya shilingi 250,000 mpaka 500,000, ambapo mteja anaweza kulipa kwa mwezi,miezi mitatu hadi mwaka kutegemeana na aina ya nyumba.
Aidha, amesema pamoja na hayo kuna service charge ya shilingi 100,000
Meneja wa Miliki wa NSSF , Augustino Paul, amewata wananchi kuchangamkia nyumba ambazo ziko Kigamboni na Tuangoma kwani bei yake ni mzuri kwenye kupangisha.
Kwa mujibu wa meneja huyo, Shirika lina nyumba 76 zilizoko Toangoma ambazo zinauzwa na kupangishwa kwa wananchi.
Amesema nyumba hizo zinapangishwa kati ya shilingi 350,000 na 400,000 kwa mwezi.
Agustino amesema Shirika pia lina nyumba 33 zilizopo Mtoni Kijichi zinazopangishwa kati ya shilingi 400,000 na 500,000.
Amesema nyumba zote ni za kisasa na zina huduma zote, na kwamba wananchi wote wanakaribishwa kuchangamkia fursa hiyo.