********************************
Na Kajubi Mukajanga
Saa sita na dakika ishirini na moja mchana wa Jumapili, Mei 10, 2020 nilizungumza na Kagina Karashani kuhusu maendeleo ya matibabu ya baba yake, Fili, na mipango ya
kumtembelea hospitali katika mazingira ya homa kali ya mapafu (Covid-19) yaliyofanya uongozi wa Hospitali ya Muhimbili (MNH) kuamua awe anaonwa na mtu mmoja tu kwasiku!.
Alikuwa amelazwa Muhimbili kwa matatizo ya moyo ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda wa miaka kadhaa.
Saa sita baadaye, saa kumi na mbili na dakika ishirini na tatu, nikapokea simu ya Kagina: “Habari ni mbaya. Mzee amefariki.”
Nilimfahamu Fili Karugahale Karashani kama rafiki mcheshi, rafiki wa kifamilia, mtu wa
masihara ambaye katika nyakati za furaha alinihakikishia kuwa ataandika wasifu wangu
pindi nitakapofariki. Nilikuwa nikimjibu kuwa mimi ndiye nitakayeandika wa kwake. Na
sasa nauandika.
Nilimfahamu pia kama mwanataaluma mahiri wa uandishi wa habari, na mkufunzi bora.
Kabla sijawa Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) tulizunguka nchi
nzima kufundisha maadili ya uandishi, stadi za uongozi katika klabu za waandishi,
mbinu za uandishi wa uchunguzi, uandishi wa habari za uchaguzi na uandishi wa
makala.
Machi 30, 2012, Fili, kama anavyojulikana kwa wengi, alikuwa mtu wa kwanza kutunukiwa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio katika Tasnia ya Habari (Lifetime
Achievement in Journalism Award) ambayo alikabidhiwa na Rais Mstaafu Jakaya
Kikwete katika Ukumbi wa Diamond Jubilee. Tuzo hizo huandaliwa na MCT na
washirika wake, na hutolewa katika kilele cha Tuzo za Umahiri katika Uandishi wa
Habari nchini, EJAT.
Alikuwa mmoja wa wanahabari Watanzania ambao usingeweza kuongelea uandishi wa
habari uliotukuka bila kuwataja. Nguli huyu alikuwa katika taaluma hii kwa miongo
mitano kama ripota, mwandishi wa makala, mhariri, mkufunzi, mtafiti na mtaalamu
mshauri wa masuala ya habari hapa nchi na ughaibuni.
Kwa maneno yake mwenyewe, alijinasibu: “I am a child of the Media” (Mimi ni mtoto wa Tasnia ya Habari).
Fili alianza maisha ya kazi kama msaidizi wa duka la vitabu mjini Dodoma mnamo
mwaka wa 1960, ambapo alijenga tabia ya kujisomea, na baadaye, kuandika.
Akahudhuria warsha ya uandishi wa habari huko Kiomboi, mkoani Singida,
iliyoandaliwa na Christian African Writing Centre iliyokuwa na makao makuu Kitwe,
Zambia, na kumaliza akiwa mwanafunzi bora darasani.
Ushindi huo ulimwezesha kupata udhamini wa kusomea Cheti cha Uandishi huko Kitwe, akiwa mmoja wa vijana
30 waliokusanywa kutoka kusini, mashariki na magharibi mwa Afrika.
Baada ya kupata cheti chake akaajiriwa kama ripota katika magazeti ya Target na Lengo, ambayo yalikuwa ndiyo kwanza yameanzishwa kwa ushirikiano kati ya mabaraza ya Kikristo ya Kenya na Tanzania.
Miaka miwili baadaye mwajiri wake akampeleka kusomea Diploma ya Uandishi
iliyoandaliwa na taasisi ya kimataifa ya wahariri, International Press Institute. Kwa mara
nyingine, Fili akawa wa kwanza katika darasa la wanafunzi 30 toka kusini na mashariki
mwa Afrika.
Wakati wa sherehe za mahafali, Mhariri wa Taifa Leo, linalochapishwa na Nation Media Group (NMG) ya Kenya akamfuata na kumweleza kuwa angependa
kumpa kazi. Fili akakubali. Hiyo ilikuwa mwaka 1964. Miezi mitatu tu baadaye, wahariri wa Daily Nation, gazeti jingine la NMG, “wakamwiba” toka gazeti lao dada. Akaingia
chumba cha habari cha gazeti lao la Kiingereza akiwa Mtanzania pekee.
Tangu hapo, Fili hakuwahi kutazama nyuma.
Kwa Fili, ukweli na usahihi (truth and accuracy) ndiyo msingi wa uandishi wa habari.
Mhariri wake wa habari pale Daily Nation, Mike Chester, alikuwa kati ya watu
waliosaidia kumfinyanga Fili kuwa gwiji wa taaluma hiyo. Chester hakuwa na masihara
kazini, na kwake, stori ilikuwa haijakamilka bila kujibu maswali “kwa nini” na “kwa jinsi
gani”.
Kati ya kazi alizofanya wakati huo ni pamoja na kuripoti machafuko ya kijamii, ukame na
njaa huko Wajir, mpakani mwa Kenya na Somalia. Baadhi ya stori alizoandika
zilimuudhi aliyekuwa Waziri wa Kilimo wa Kenya wakati huo, Jeremiah Nyagah. Lakini
ukweli na usahihi ukamwokoa, hakufanywa chochote.
Aliandika pia matatizo ya wananchi huko Baringo, jimboni kwa Daniel arap Moi, wakati
huo akiwa Makamu wa Rais na Waziri wa Mambo ya Ndani. Mzee Moi hakupendezwa
sana na stori za Fili, na akaagiza aletwe kwake. Alipofika, akamtazama Fili kwa
mshangao toka chini hadi juu na kumaka, “Oh, huyu ndiye Karachani – nilidhani ni
Mhindi! Kwenda!”
Awali, lengo lilikuwa kumsweka korokoroni. Ukweli na usahihi vikamwokoa.
Tom Mboya alipouawa, Fili ndiye aliyeliandikia Daily Nation mkasa huo.
Mwaka 1967 akahamishiwa Dar es Salaam kwa mwaka mmoja na kuendelea kupeleka
Nairobi stori kemkem. Asilimia kubwa ya stori za Tanzania zilizochapishwa ukurasa wa
mbele wa Daily Nation wakati huo ziliandikwa na Fili.
Aliporudi Nairobi, Fili alikwea vidato toka ripota hadi mwandishi mkuu wa habari za
Bunge, akawa pia mwanasafu, na baadaye Mhariri-usu/Msanifu Habari (Sub-editor).
Alikuwa pia akiandika safu kuhusu masuala ya Tanzania katika gazeti hilo lililoongoza
kwa mauzo Afrika Mashariki.
Baadaye akaacha kazi na kujiunga Chuo Kikuu cha Dar e Salaam na kupata shahada
yake ya kwanza mwaka 1978, kisha shahada ya uzamili toka Chuo Kikuu cha Queens,
Canada, mwaka 1981.
3
Baada ya chuo kikuu Fili akajiunga na gazeti la Daily News kabla ya kuwa mkufunzi
katika Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania, TSJ. Akiwa mkufunzi, akawa pia
akiandikia majarida na taasisi za nje zikiwamo jarida maarufu la Africa Now na shirika la
Inter Press News Agency (IPS). Kwa bahati mbaya, jambo hili lilitafsiriwa na wakubwa
wake kuwa ni “kufanya kazi mbili”, japo kwake yeye aliona ni njia ya kuwaonyesha
wanafunzi kwa vitendo jinsi uandishi bora ulivyo. Alipoona anasakamwa sana, akaacha
kazi na mara moja IPS wakamchukua na kumpa kazi Roma, Italia, na baadaye
wakampeleka Harare, Zimbabwe, kama Mkuu wa Kituo (Bureau Chief).
Aliporudi Tanzania 1989 akawa Mhariri mwanzilishi wa Business Times, akiwa na kina
Rashid Mbuguni, Narendra Joshi, Ali Chimbyangu na Richard Nyaulawa.
Mwaka 1991 Fili Karashani aliajiriwa kama Mhariri wa Southern Africa Economist jijini
Harare, kabla ya kurudi Dar es Salaam na kuwa Mhariri mwanzilishi wa The Guardian
na baadae Sunday Observer.
Mnamo 2004 hadi 2005 alikuwa The Citizen kama Mhariri wa Mafunzo.
Katika miaka ya mwisho ya maisha yake, Fili Karashani , ambaye waandishi wengi
wamepitia mikononi mwake akiwa mhariri na mwalimu, aliendelea kutoa mafunzo ya
uandishi, hususan uandishi wa habari za uchunguzi, makala, na maadili. Alitoa pia
huduma kama mtaalamu mshauri wa masuala ya habari, huku akichangia katika
majarida ya kitaaluma yakiwamo Scribes la MCT na The Global Journalist la Shule Kuu
ya Uandishi wa Habari ya Chuo Kikuu cha Missouri, Marekani.
Vitabu alivyoandika au kushiriki kuandika ni pamoja na: To Write or Not to Write –
Ethical Concerns in Journalism; Poverty Reporting – A Manual for Tanzanian
Journalists; Media Ethics: Duties and Responsibilities; Feature Writing Manual na
Investigative Journalism Practice in Tanzania.
Fili Karashani alipata kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wanahabari wa Kenya (Kenya
Union of Journalists) na katika miaka yake ya mwisho alikuwa mwenyekiti wa Kituo cha
Habari, Tanzania Press Centre kabla ya kupatwa na matatizo ya kiafya.
Fili Karashani alizaliwa Agosti 23, 1938 mjini Dodoma. Baba yake alikuwa Yakobo
Kagina, mchungaji wa kanisa la Anglikana, na mama yake aliitwa Blandina.
Fili na mkewe, Geraldina, walijaaliwa watoto watano: Magezi, Baraka, Kagina, Koku na
Bahati. Baraka, aliyechukua kazi ya baba yake ya uanahabari, alishatangulia mbele ya
haki. Fili pia ameacha wajukuu wanane.
Mungu ailaze pema roho ya marehemu Fili Karugahale Karashani—Amina.